MKUU wa Mkoa wa Mwanza, Mhe. Adam Malima amewaagiza wakurugenzi wa halmashauri zote mkoani humo kutenga na kuwasilisha fedha za kutekeleza afua za lishe kwa wakati ili kuepuka udumavu kwa watoto na kutengeneza kizazi cha watu wenye ufahamu.
Mhe. Malima ametoa agizo hilo Mkoani humo leo Februari, 10, 2023 wakati akizungumza kwenye kikao cha tathmini ya utekelezaji wa mkataba wa lishe na utambulisho wa mfumo wa M-Mama ambao lengo lake ni kuokoa maisha ya wanawake wajawazito, waliojifungua na watoto wachanga wanapokuwa na dharura za kiafya.
Agizo hilo la Mhe. Malima amelitoa baada ya Afisa Lishe wa Mkoa huo, Sophia Lazaro kutoa taarifa ya utekelezaji wa afua za lishe kuanzia Julai hadi Desemba 2022 iliyobainisha kwamba miongoni mwa changamoto wanazokabiliana nazo kuwa ni pamoja na baadhi ya halmashauri kutotoa fedha zilizotengwa na serikali kwa wakati ili kuwezesha utekelezaji wa afua za lishe pia hazilingani na idadi ya watoto.
Ameziagiza kila halmashauri kutoa fedha zote za utekelezaji wa afua za lishe ifikapo Juni 30 mwaka huu kwa kufuata miongozo iliyopo kwani kila kiongozi wakiwemo wakurugenzi wanapaswa kulipa kipaumbele suala la lishe ili kutengeneza taifa lenye watu watakaoendeleza taifa lakesho .
“Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan ameipa kipaumbele ajenda hii ya lishe tangu akiwa Makamu wa Rais na sasa ni Rais, ili kutengeneza taifa bora la kesho kwa sababu watoto wanaokabiliwa na changamoto ya utapiamlo nao wanategemewa kuendeleza nchi hapo baadaye ndiyo maana serikali inawajali ili waweze kuimarika kiafya, hivyo sitarajii kuona kiongozi yeyote hasa sisi ambao tunamsaidia Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan Kumkwamisha kwa namna yoyote ile,”amesisitiza Mhe. Malima.
Katibu Tawala wa Mkoa huo, Balandy Elikana amesema” Kwa kipindi hiki ambacho kimebaki cha miezi minne ya utekelezaji wa bajeti ya mwaka 2022/2023 tuchukue hatua zinazostahili kuhakikisha tunatekeleza makubaliano yaliyopo kwenye mkataba”.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.