Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Adam Malima amehimiza elimu zaidi kwa wakulima wa zao la Pamba ili malengo yatimie ya kumkomboa mkulima kiuchumi na Mkoa huo kuwa kinara wa zao hilo hapa nchini.
Akizindua msimu wa kilimo cha Pamba Wilayani Sengerema kata ya Nyampande, Mkuu huyo wa Mkoa amesema lazima kuwepo na mabadiliko yenye tija kwenye Pamba kwa hekari moja kutoa kilo 500 hadi 600.
"Tuache kutumia kilimo cha uzoefu na badala yake tufanye kilimo cha kisasa kwa kuzingatia mbegu bora, mbolea ya MPK kutoka Minjingu na upandaji wa kutumia sentimita 60 mstari kwa mstari na mche kwa mche sentimita 30", amesisitiza Mhe. Malima
Aidha ametangaza vita kwa wale wote watakaobainika kusambaza pembejeo zisizo na ubora kwani wanachangia kumpa mzigo wa umasikini mkulima.
Kuhusu bei ya Pamba, Mkuu huyo wa Mkoa amebainisha mwelekeo mzima unategemeana na soko la Dunia na bei inabadilika kila wakati kutegemeana na wingi au upungufu wa upatikanaji wake na kuwataka wanasiasa kuwacha kutumia eneo hilo kujinufaisha kisasa.
Amesema, Serikali imechagua Mkoa wa Tabora na Katavi kuwa mzalishaji wa mbegu za Pamba ambazo zitatayarishwa kitaalamu ili ziwe na matokeo chanya kwa mkulima na mkakati wa kudhibiti bei ukiwa unafanyiwa kazi.
Mkoa wa Mwanza msimu huu umevuna kilo milioni 15 huku bei elekezi ikiwa Sh 1560 na kupanda hadi 2100.
Simiyu ndio Mkoa unaoongoza kwa uzalishaji wa zao la Pamba hapa nchini.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.