RC MTANDA AAGIZA KUFUNGWA MFUMO WA KUKUSANYA MAPATO ILI KUDHIBITI UPOTEVU FEDHA BUDUSHI HC
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda amemuagiza Katibu Tawala Mkoa kushirikiana na Mganga Mkuu wa Mkoa kuhakikisha ndani ya siku 14 wanaweka mfumo wa makusanyo na matumizi ya fedha kwenye Kituo cha Afya Budushi kilichopo kata ya Sumve wilayani Kwimba.
Ametoa agizo hilo mapema leo Septemba 14, 2024 wakati akifanya ukaguzi wa huduma za afya kwenye kituo hicho na kubaini kuwapo kwa mfumo wa makusanyo na matumzi wa makaratasi badala ya Mfumo wa kisasa wenye ufanisi na unaodhibiti upotevu wa mapato (GOTHoMIS).
Sambamba na hilo, Mhe. Mtanda amemtaka katibu tawala kwa kushirikiana na OR -TAMISEMI kuandaa mafunzo kwa Wakurugenzi wa Halmashauri, Waganga Wakuu wa Wilaya na maafisa TEHAMA ili kuwajengea uwezo wa namna ya kutumia mfumo huo kwa tija na akaahidi kuwa mgeni rasmi kwenye ufunguzi wa mafunzo hayo.
Aidha, ametoa rai kwa Mganga mkuu wa wilaya hiyo kuwa mbunifu na mwenye maamuzi ya haraka katika kufunga mifumo na vifaa tiba na visaidizi kwenye vutuo vya kutolea huduma ili malengo ya serikali ya kuboresha huduma za afya yaonekane mapema.
Akikagua ujenzi hususani kwenye jengo la Mama na Mtoto na kichomea taka ameagiza kasi ya ujenzi iongezwe ili hadi kufikia septemba 30, 2024 wakamilishe na huduma kwa wananchi zaidi ya elfu 17 ziendelee kutolewa katika hali ya ubora na kuwapunguzia msongamano kwenye hospitali ya Kanisa waliyokua wanapata huduma siku za nyuma.
Awali, akiwasilisha taarifa Mganga mfawidhi wa Kituo hicho Paul Kanga amesema mradi wa ujenzi wa kituo hicho umepokea kiasi cha Tshs. 656.4 milioni ambapo Tshs. 300 Milioni kutoka mapato ya ndani ya Halmashauri na Tshs. 356.4 kutoka TASAF ambayo inahusisha na Tshs. 16.5 Milioni za nguvu za wananchi ambao wamenunua pia eneo kwa Tshs. 8 milioni.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.