RC MTANDA AIPONGEZA WIZARA YA KATIBA NA SHERIA KUENDELEA KUFIKIKA
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda ametoa pongezi kwa Wizara ya Katiba na Sheria kwa kuendelea kuwafikia wananchi kwa ukaribu zaidi na kutatua changamoto zao pamoja na utoaji wa elimu kuhusu masuala ya sheria.
Mkuu wa Mkoa ameyasema hayo mapema leo Machi 03, 2025 wakati alipokuwa akifungua mafunzo ya Wajumbe wa Kamati ya Usalama Mkoa kuhusu Elimu ya Uraia na Utawala Bora ambapo yamewakutanisha Kamati ya Usalama ya Mkoa, Kamati za Usalama za Wilaya, baadhi ya Wataalam wa Halmashauri na Watendaji wa Kata zote za Mkoa wa Mwanza.
Mkuu wa Mkoa amesema uchangamanaji wa Wizara hiyo na Wananchi umekuwa na tija kubwa kwa jamii kwani imekuwa msaada mkubwa kwa wananchi wenye changamoto mbalimbali za kisheria ambapo wamekuwa wakipatiwa ufumbuzi.
kupitia Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia (Mama Samia Legal Aid Campaign) iliyozinduliwa tarehe 18 Februari, 2025 hapa Mkoani Mwanza lakini pia Kamati ya msaada wa kisheria na leo mafunzo haya, yote haya yanaifanya Wizara hii kuendelea kuonekana.
“Hatua hii imesaidia Serikali kuendelea kuaminiwa na Wananchi, kuimarisha amani na mshikamano ndani ya jamii”.
Kadhalika ameishukuru Wizara ya Katiba na Sheria kwa kuona umuhimu wa kuendesha mafunzo hayo na ni wazi kuwa mafunzo hayo yataongeza uelewa na tija kuhusu masuala ya Uraia na Utawala Bora.
“Ninafahamu kuwa wote tunaoshiriki mafunzo haya tunawawakilisha viongozi walio chini yetu na ni imani yangu kuwa mafunzo haya yatatusaidia kuongoza kwa kuzingatia misingi ya Utawala Bora”.
Akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria, Mkurugenzi Msaidizi wa Ufuatiliaji Haki, Bw. Lawrence Kabigi amesema Mafunzo hayo ya elimu ya uraia na Utawala bora yanayowalenga viongozi kuanzia ngazi ya Mkoa, Wilaya hadi Halmashauri yana lengo la kuwajengea uwezo viongozi na wataalamu kufanya kazi kwa kuzingatia sheria za nchi
“Wizara ya Katiba na Sheria imekuwa kinara wa kutumia 4R za Mhe. Rais yaani Maridhiano, Ustahimilivu, Mabadiliko, na Kujenga upya ili kuwepo na Utawala bora na wananchi kuishi kwa amani na upendo miongoni mwao”.
Mafunzo ya Elimu ya Uraia na Utawala Bora hadi sasa yameshafanyika kwenye mikoa kumi na moja (11) kwa kuwatumia watoa mada kutoka Wizara ya Katiba na Sheria, Tawala za Miko na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Jeshi la Polisi na Tume ya haki za binadamu na Utawala bora, Na kwa sasa mafunzo hayo yanaendelea kutolewa kwenye mikoa sita (6) ukiwemo Mkoa wa Mwanza.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.