RC MTANDA ATAKA MAUDHUI YA KUCHAGIZA MAENDELEO KWA VITENGO VYA MAWASILIANO YA SERIKALI
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda amevitaka vitengo vya Mawasiliano ya Serikali ngazi ya Mkoa na Halmashauri kuandika habari zenye maudhui bora ya kuhamasisha maendeleo na utatuzi wa kero za wananchi.
Mhe. Mtanda ameyasema hayo mapema leo Julai 17, 2024 baada ya kupokea kikombe na cheti cha ushindi wa nafasi ya pili kwa ngazi za Mikoa kilichotolewa na Waziri wa Habari Mhe. Nape Nnauye kwenye Kongamano la Habari lililofanyika jijini Dar es Salaam Juni mwaka huu.
Mhe. Mtanda amesema katika kuhabarisha umma jamii inatamani kujua ni kitu gani Serikali inafanya kwa wananchi hivyo basi ni lazima vitengo hivyo vijikite katika kuelezea miradi ya maendeleo inayofanywa na Serikali kw ajili ya kuboresha huduma kama za maji, miundombinu ya barabara, elimu na afya.
Aidha, amesema ziara za viongozi zimekuwa na tija sana kwa jamii hususani usikilizaji kero za wananchi pamoja na kuzitatua kama ambavyo yeye binafsi anaendelea nazo hivyo vitengo vya mawasiliano vinapaswa kuonesha shida na madhila wanayopitia wananchi na jinsi gani zinatatuliwa.
Vilevile, Mhe. Mtanda ameagiza vitengo vya mawasiliano katika Halmashauri zote 8 za mkoani humo kuchapa kazi katika kuhakikisha wanahabarisha umma juu ya yote yanayoendelea kwenye maeneo yao huku akionesha kiu yake ya kupata habari za wananchi wanaoishi kwenye visiwa vya Ukerewe.
Akiwasilisha kikombe na cheti cha ushindi kwa Mhe. Mkuu wa Mkoa, Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Paulo Zahoro amebainisha kuwa ushindi huo (nafasi ya 2 kati ya mikoa 26 ya Tanzania Bara) umetokana na uhabarishaji umma mzuri na akaahidi kuendelea kuboresha zaidi.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.