RC MTANDA ATOA WITO KWA WANANCHI KUITUMIA VYEMA SIKU YA MWISHO KUJIANDIKISHA KWENYE DAFTARI LA KUDUMU LA WAPIGA KURA
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda ametoa wito kwa wananchi wa Mkoa huo kutumia vyema siku ya mwisho ya kujiandikisha na kuboresha taarifa zao kwenye daftari la kudumu la wapiga kura.
Mhe. Mtanda ametoa wito huo mapema leo Agosti 27, 2024 wakati akiboresha taarifa zake kwenye daftari la kudumu la wapiga kura katika kituo cha Isamilo Kaskazini kilichopo kata ya Isamilo Wilayani Nyamagana.
Amesema, kuwa na kitambulisho cha kupigia kura ndio silaha ya demokrasia kwani kitampa mwananchi fursa ya kuchagua kiongozi amtakaye kwenye uchaguzi mkuu wa Madiwani, Wabunge na Rais.
Aidha, amebainisha kuwa muitikio wa wananchi mkoani humo kwenye kujiandikisha ni mkubwa na akafafanua kwamba mwananchi atakayefika kwenye foleni ya kujiandikisha kabla ya muda wa kufunga vituo atapata haki hiyo.
Halikadhalika, amebainisha kuwa zoezi hilo ni la muda mfupi sana kwani ndani ya dakika tatu mwananchi anakua ameshapata kitambulisho cha kupigia kura na anaondoka kwenda kuendelea na shughuli zake.
Vilevile, ametumia wasaa huo kutoa wito kwa wananchi mkoani humo kujituma katika shughuli halali za kujitafutia kipato badala ya kukaa kwenye vijiwe kubishana na kuzungumza mambo yasiyo na msingi kwani fursa zipo nyingi kinachotakiwa ni kujibidiisha tu.
Zoezi la uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura mkoani Mwanza lilianza Agosti 21,2024 na linatarajiwa kukamilika leo Agosti 27, 2024 saa 12 jioni ikiwa na kaulimbiu isemayo "Kujiandikisha kuwa Mpiga Kura ni Msingi wa Uchaguzi Bora".
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.