RC MTANDA AWATAKA NSSF KUENDELEA KUSHUGHULIKA NA CHANGAMOTO ZA WASTAAFU
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda ametoa wito kwa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) kuendelea kuwajengea uwezo wastaafu watarajiwa na kushughulika na utatuzi wa changamoto zinazowakabili wazee.
Mhe. Mtanda ametoa wito huo leo Mei 28, 2024 wakati akizungumza na wastaafu watarajiwa ambao ni wanachama wa mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) katika ukumbi wa Benki Kuu ya Tanzania (BOT) Mwanza.
Mtanda amesema kwa uzoefu aliokuwa nao kupitia uenyekiti wake wa Kamati ya Bunge ya Maendeleo ya Jamii amebaini kuwa hifadhi za jamii haziwezi kujitenga na maslahi ya wazee kwa kuhakikisha wanajengewa msingi wa kutoa pensheni kwa kundi hilo.
"Semina hii inafanyika kwa madhumuni ya kuwakumbusha wanachama kujiandaa kupunguza uwekezaji kwa kujiandaa kuondoka na kwenda kwenye maisha mapya ambayo ni ya kuishi bila mshahara na uchumi pamoja na hadhi ndogo tofauti na sasa." Mhe. Mtanda.
Aidha, amewataka wastaafu hao watarajiwa kujiandaa na kuwa na uamuzi kwa kuwa na vitega uchumi kabla ya kustaafu na kupanga wapi wanakusudia kwenda kuishi kwani maisha ya mjini yanatofautiana na ya kijijini kwani yana asili tofauti ya mahitaji na aina ya biashara au shughuli za kuwekeza.
Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu NSSF nchini Robert Kadege ameshukuru uongozi wa Mkoa na Waajiri waliowaruhusu wastaafu 400 wataopata elimu ya juu ya kustaafu bila hofu, mafao na ukokotozi wa mafao pamoja na masuala ya afya kwa siku mbili.
Emanuel Kahensa, Meneja NSSF Mwanza ametumia wasaa huo kuwashukuru wanachama hao kwa uaminifu na kukubali kupata mafunzo hayo na akaahidi kuwapitisha kwenye mafunzo ya kuwajengea uwezo wa namna gani wataenda kuishi kwa furaha baada ya kustaafu.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.