RC MTANDA: UZINDUZI MV MPUNGU NI ISHARA YA MAENDELEO SEKTA YA USAFIRISHAJI MAJINI
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe Said Mtanda amesema uzinduzi wa wa Meli kubwa ya mizigo ya MV Mpungu yenye uwezo wa kubeba tani 1,000 sawa na magari ya kubeba mizigo (Trailer 21) ni ishara ya maendeleo na ukuaji wa sekta ya usafirishaji majini katika Mkoa wa Mwanza.
Mkuu wa Mkoa ameyasema hayo leo mei 21,2025 wakati wa uzinduzi wa Meli hiyo ya MV Mpungu uliofanyika katika Bandari ya Mwanza Kusini ambapo amesema kuzindua meli hiyo katika Mkoa wa Mwanza ni uamuzi sahihi kwa kuwa ni Mkoa wa Kimkakati na kiuchumi.
“Ni matarajio ya wengi kuwa kuzindua kwa meli hii kubwa ya mizigo ya MV Mpungu itakata kiu ya Wafanyabiashara waliokuwa wakisubiri kwa hamu meli kubwa ya kusafirisha mizigo kutoka Mwanza kwenda Portbell, Uganda”. Amesema.
"Uwepo wa meli hii utachangia kukua kwa sekta ya usafirishaji majini na kukua kwa pato la Taifa." Ameongeza Mkuu wa Mkoa.
Kadhalika, Mkuu wa Mkoa amesema juhudi kubwa sana zimefanywa na Serikali ya awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuimarisha usafiri wa majini kwa ujenzi wa vivuko vitano (5) vyenye thamani ya Sh. Bilion 28.
Pia amesema serikali imetoa fedha takribani shilingi Bilioni 18.6 kugharamia mradi wa upanuzi wa Bandari ya Mwanza Kaskazini ambao umefikia Asilimia 58. Ujenzi wa Meli Mpya ya MV Mwanza itakayogharimu 123 Bilioni, yenye uwezo wa kubeba abiria 1,200, tani 400 za mizigo magari madogo 20 na malori 3, mradi umefikia asilimia 98.
“Lakini pia tuna ujenzi wa Makao Makuu ya Kituo cha Utafutaji na Uokozi katika Ukanda wa Ziwa Viktoria (MRCC –Regional Maritime Rescue Coordination Centre), unaogharimu 64.99 Bilioni na umefikia Asilimia 84”. Amefafanua.
Akisoma taarifa kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka za Bandari, Meneja wa Bandari Ziwa Victoria Bw. Erasto Ligenge amesema bandari ya Mwanz kusini ni moja ya vituo muhimu vya kimakakatu ambapo ina uwezo wa kuhudumia tani laki mbili kwa mwaka.
Aidha, amesema uzinduzi wa meli hiyo mpya ya mizigo itasaidia kubeba mizigo mingi kwa wakati mmoja ambapo kwa safari moja mizigo zaidi ya tani moja itasafirishwa kadhalika itapunguza safari za muda mrefu kwa njia ya barabara pamoja na kushusha wastani wa gharama za usafirishaji.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.