RC MWANZA AHIMIZA USHIRIKIANO NA WADAU WA UJENZI.
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhe. Said Mtanda, amesema dhamira ya Serikali ni kuendelea kushirikiana na wadau wa sekta ya ujenzi ili kuhakikisha wananufaika na miradi mikubwa inayotekelezwa na Rais Samia Suluhu Hassan mkoani humo.
Akizungumza katika hafla ya wadau wa sekta ya ujenzi, Iliyoandaliwa na kampuni ya magic builders international limited Tanzania Mhe. Mtanda amebainisha kuwa Serikali inatambua mchango wa mafundi katika maendeleo ya miundombinu na itahakikisha maslahi yao yanalindwa.
Pia ameahidi kushughulikia changamoto ya mafundi kucheleweshewa malipo pindi wanapomaliza kazi kwenye taasisi mbalimbali wakiwemo watu na makampuni.
Katika hafla hiyo mkuu wa mkoa wa Mwanza amekabidhi vifaa vya shule yakiwemo madaftari kwa watoto zaidi ya 300 wa mafundi hao, ambavyo vimetolewa na kampuni ya magic builders international limited ili kuongeza chachu kwa watoto hao kupenda elimu.
Kwa upande wao, mafundi wamezungumzia utayari wa kushirikiana na Serikali katika nyanja mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kushiriki uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu.
Aidha, wameiomba Serikali kurasimisha kundi lao, likiwemo la mafundi rangi, ili waweze kupata fursa kama mikopo na huduma nyingine zinazotolewa kwa makundi mengine kama kundi la waendesha bodaboda.
Katika hotuba yake, Mtanda pia amewaonya vijana wanaoeneza dhana potofu kuwa mtu anaweza kupata pesa bila kufanya kazi ambapo amesisitiza kuwa huo ni upotoshaji mkubwa kwa vijana ambao ndiyo nguvu kazi ya Taifa.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.