Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Mhandisi Robert Gabriel amewaongoza Wananchi wa Mwanza katika kumbukumbu ya Siku ya Mashujaa na kuwataka kuendelea kuwaenzi Mashujaa kwa vitendo ikiwemo uadilifu wa kulinda rasilimali za Taifa.
Sherehe hizo zilizofanyika leo katikati ya Jiji la Mwanza eneo la mzunguko uliopo Mnara wa Mashujaa hao waliopigana Vita Kuu ya Kwanza na ya Pili ya Dunia, Mkuu huyo wa Mkoa amesema haitakuwa na maana kuwakumbuka Mashujaa hao huku Wananchi wakiwa hawana uzalendo na Taifa lao.
"Hawa Mashujaa wetu licha ya kupigana Vita hizo walitumia silaha duni dhidi ya Wakoloni waliokuwa na silaha za kisasa lakini walitambua wanapigania Taifa lao hivyo walijitoa muhanga huu ni mfano unaotakiwa kuendelea kuigwa kwa sisi tulio hai" Mhe Gabriel.
Katika Sherehe hizo, Mzee Bega Maliba mwenye Umri wa Miaka 104 ambaye ni askari wa zamani aliyepigana Vita kuu ya Pili ya Dunia, alikua kivutio kwenye sherehe hizo na alipewa heshma ya kuweka Shoka kwenye Mnara wa Mashujaa.
Askari huyo wa zamani anayeishi Wilayani Ukerewe amesema kilichowapa heshma na kufanya vizuri enzi zao ni nidhamu ya hali ya juu waliyokuwa nayo wakiwa jeshini.
Aidha, Mkuu Mkoa ameweka Mkuki na Ngao kwenye Mnara kama ishara ya kuwakumbuka Mashujaa hao huku Viongozi wengine wa Serikali, Dini, Vyombo vya Ulinzi na usalama pamoja na Mtemi wa Mwanza Aron Nyamilonda wakiweka mashada ya maua,Sime na silaha za jadi.
Sherehe za kumbukumbu ya Mashujaa Kitaifa zimefanyika Mkoani Dodoma zikiongozwa na Mhe Rais Samia Suluhu Hassan.
Mashujaa hao wanaokumbukwa kila Julai 25 wamepigana Vita kuu ya kwanza iliyoanza mwaka 1914 hadi 18 na Ile ya Pili iliyopiganwa kuanzia mwaka 1939 hadi 45.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.