SERIKALI KUNUNUA MTAMBO RASMI WA KUSAFISHA ZIWA VICTORIA
Serikali imedhamiria kununua mtambo maalum wa kusafisha ziwa victoria lililoathirika na gugumaji jipya ambalo limekuwa tishio kwa shughuli za uvuvi na usafirishaji kwa wananchi.
Kauli hiyo imetolewa leo Mei 10, 2025 na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda alipokua akizungumza na Wananchi waliokuwa wakisubiri huduma ya usafiri wa kivuko katika eneo la Busisi Wilayani Misungwi.
Mkuu wa Mkoa amesema mpaka sasa fedha tayari zimeshatengwa na taratibu za manunuzi zimeshaanza na muda si mrefu mtambo huo utawasili na kazi hiyo ya uvunaji wa magugu maji itaanza mara moja.
“Kwanza tunamshukuru sana Mhe. Waziri Mkuu kutokana na kikao chake ndio tunaona matunda haya leo, lakini pia Mhe. Rais kwa kuidhinisha fedha”. Mhe. Mtanda.
Aidha, Mhe. Mtanda amesema Serikali imedhamiria kuhakikisha Wafugaji wa Samaki kwa njia ya vizimba hawaathiriki na madhara ya magugu maji kwa kuwa serikali inafanya jitihada za makusudi kuhakikisha wanadhibiti hilo kwa teknolojia ya kisasa.
Sambamba na hayo Mkuu wa Mkoa amewataka wananchi hao kuwa na subira kutokana na changamoto ya usafirishaji kwa njia ya vivuko kwa kuwa sasa daraja la JPM liko hatua za umaliziaji na wakati wowote kuanzia sasa litazinduliwa rasmi.
“Mwenye macho haambiwi tazama, sasa daraja linakamilika tuendelee kuvuta subira, siku si nyingi changamoto hii itakua imekwisha kabisa”. Ameongeza Mkuu wa Mkoa.
Katika ziara hiyo Mkuu wa Mkoa amembatana na Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhandisi Cyprian Luhemeja ambaye amesema ushirikiano uimarishwe kazi ifanywe kwa pamoja baina ya Wataalamu wa Kisekta, Wavuvi, pamoja na Wafugaji wa vizimba ili ziwa libaki salama na matokea mazuri na ya muda mrefu yapatikane.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.