Serikali imesema itaendelea kuboresha utendaji kazi wa Mahakama ili kuiwezesha kuendelea kutoa haki kwa wananchi na kuimarisha mnyororo wa utoaji haki.
Hayo yameelezwa jijini Mwanza leo Aprili 12,2023 na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Isdor Mpango alipomwakilisha Mheshimiwa Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kwenye mkutano wa tathmini ya utendaji wa mapitio ya nusu ya kwanza ya mpango mkakati wa mahakama 2020/21 hadi 2024/2025.
Ameongeza kuwa ufanisi wa shughuli za utoaji haki nchini ni nguzo muhimu ya kulinda amani na utulivu uliopo, kukuza utawala wa sheria pamoja na shughuli za kiuchumi, biashara na uweezaji
"Majaji muendelee kufanya kazi kwa uadilifu ili kuwawezesha watanzania kupata haki kwa mujibu wa sheria, ucheleweshwaji wa mashauri unaongeza gharama si tu kwa wadau bali hata kwa uchumi wa taifa hivyo ni wajibu wa mahakama kuhakikisha wananchi wanapata huduma za mahakama kwa gharama nafuu," ameagiza.
Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. pauline Gekul amempongeza Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuunga
Mkono juhudi za utendaji kazi wa muhimili wa mahakama nchini hususan kwa kuiwezesha mahakama kifedha katika kutekeleza majukumu yake kwani muhimili huo ni moja ya nguzo ya kudumisha amani na utamaduni wa nchi.
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe.Adam Malima amemshukuru Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe.Prof. Juma na uongozi wa mahakama kwa kufanyia mkutano huo muhimu sana katika kuhakikisha utendaji kazi wa mahakama unaimarika mkoani humo.
"Kwa niaba ya wananchi wa Mkoa wa Mwanza tunashukuru sana pia tunakushukuru sana Mhe. Makamu wa Rais Dkt.Mpango kwa ujio wako mgeni njoo mwenyeji apone hivyo naomba washiriki wote wa mkutano huu mkimaliza mkutano msiondoke bila kutembelea vivutio vilivyopo mkoani mwetu ikiwemo saa nane na jiwe linalocheza lililoko Wilaya ya Ukerewe," ameeleza Mhe. Malima.
Naye, Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe.Prof Ibahim Juma amesema mkutano walioufanya Novemba 10,2014 waliamua kupambana na changamoto zinazokabili mfumo wa utoaji haki ikiwemo ucheleweshaji mkubwa katika utatuzi wa migogoro,vitendo vya rushwa na ukiukwaji wa maadili ili kuhakikisha wananchi wanaridhika na huduma wanazozitoa.
"Ili kuboresha huduma tunazozitoa tumetunga kanuni mpya zaidi ya 75 katika kamati mbalimbali tunachopaswa kujiuliza sio kanuni tulizozitunga tujiulize je ndani ya hizo kanuni zimeleta mabadiliko gani?" amehoji.
Kwa mujibu wa Mhe.Pro.Juma mkutano huo utasaidia kuongeza ufanisi wakati wa utekelezaji wa shughuli za mahakama.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.