Serikali yawataka wananchi kutojitenga na jukumu la kuondoa changamoto Shuleni Serikali imesema inatambua ukweli wa namna taasisi zake hususani sekta ya elimu ilivyo na changamoto zinazokwamisha upatikanaji wa haraka wa maendeleo lakini haiwezi kuziondoa kwa wakati mmoja.
Hivyo imewataka wananchi kutambua ushiriki wao wa kuchangia fedha za miradi mbalimbali shuleni utawezesha Serikali kufanikisha kuziondoa changamoto hizo kwa urahisi na watoto wao kupata elimu bora kwa shule za umma.
Kauli hiyo imetolewa na Afisa Elimu Taaluma Mkoa wa Mwanza, Joseph Ngoseki, aliyemwakilisha Afisa Elimu mkoa huo, Michael Ligola katika mdahalo wa wazi kujadili huduma ya elimu inavyotolewa katika shule za msingi na sekondari za umma.
Mdahalo huo ulioandaliwa na Taasisi ya Ilemela District CSOS Network (ILEDICNET) ulihudhuria na vongozi mbalimbali wa Serikali, wadau wa elimu na wananchi ambapo walisema bado shule za serikali zinakabiliwa na changamoto kadhaa zikiwamo ni uhaba wa vyumba vya madarasa ya awali na msingi.
Pia upungufu wa matundu vya vyoo, vitabu vya kiada, madawati, kukosekana kwa huduma ya maji shuleni, chakula, usiri juu ya mapato na matumizi ya shule, mahusiano mabaya kati ya jamii na walimu, shule kutokuwa na vifaa vya kujikinga na majanga ya moto, upungufu wa walimu sambamba na walimu kutopandshwa madaraja na mengine mengi.
Akijibu hoja za wachangiaji, Ngoseki alisema ni kweli shule za Serikali zina mapungufu yaliyotajwa lakini si rahisi kuondoa changamoto hizo kwa wakati mmoja ispokuwa zitakwisha endapo wananchi watajitolea kwa nafasi yao kwa kuchangia fedha.
“Wananchi wanapaswa kuelewa hizi shule ni zao na ndio maana zinasimamiwa na kamati au bodi za shule ambaqpo wajumbe wake wanatokana na wananchi hao hao, sasa ili tuziondoe changamoto hizo ni lazima tushirikiane kwa pamoja, mfano hivi sasa kuna upungufu wa vyumba vya madarasa kinachotakiwa ni wananchi wajenge boma na serikali itaezeka.
“Sasa jamii ikisubiri Serikali ifanye kila kitu tutachelewesha maendeleo ya sekta ya elimu, binafsi naipongeza Halmashauri ya Ilemela ambayo viongozi wake na wananchi wamejipangia utaratibu wao kwamba katika kumaliza kero ya madarasa, wananchi wanajenga msingi, mbunge anayesimamia boma na halmashauri inaezeka, leo hii Mkoa wa Mwanza tunawatolea mfano kwa kuwa na miradi mengi.
“Najua kuna mapokeo hasi kwa wananchi juu ya kauli ya elimu bure kitendo ambacho kinasababisha kutochangia, usahihi ni kwamba Serikali imesema elimu ni bure bali ni elimu msingi bila malipo, hivyo wananchi wanapaswa kutambua michango ya maendeleo katika shule zao ipo, ni muhimu kujenga nyumba za walimu, vyoo pia wana jukumu la kusimamia na kuhoji fedha zinazoletwa na Serikali kupitia kamati za shule,”alisema.
Naye Meya wa Halmashauri ya Ilemela, Renatus Muruga, alisema hadi sasa halmashauri hiyo imeweza kujenga misingi 92 ya vyumba vya madarasa, maboma 90 yamekamilika na kati ya hayo 31 yameezekwa ambapo Mbunge wa Jimbo la Ilemela, Mhe. Angelina Mabula (CCM) ametoa matofali 485,000 kwa vyumba vya madarasa, nyumba za walimu na vyoo.
Muruga aliwataka wananchi kuelewa maana ya Serikali ni wewe na mimi ikiwa na maana watu wote hivyo kila mmoja anapaswa kuwajibika kwa nafasi yake.
Kwa upande wa Diwani wa Kata ya Buhongwa, Sarah Ngwani (CCM) alipongeza taasisi ya Iledicnet kwa kufanya utafiti na kuandaa mdahalo huo ambao umesaidioa Serikali kutambua changamoto zinazokabili shule zake na kuwataka wananchi kuungana na viongozi kusaidiana kuzitatua.
Naye Mratibu wa Iledicnet , Nicas Nibengo, alisema ikiwa serikali itaweza kutatua mapunfufu yaliyopo katika shule zake, hakika zitaleta ushindani mkubwa dhidi ya shule binafsi.
“Vile vile tunashauri jamii ielimishwe juu ya kuchangia kwani imebainika imepokea kauli ya Serikali elimu bure kwa mtazamo tofauti, wito kwa Serikali kuweka mikakati ya kuhakikisha vyumba vya madarasa vinapatikana ili kuepusha wanafunzi kulundikana katika darasa moja, vile vile kuongeza walimu wa kutosha katika shule zake, vinginevyo ubora wa elimu utaendelea kushuka.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.