Serikali imezindua rasmi ujenzi wa vivuko viwili vya kisasa vitakavyofanya safari za kusafirisha abiria , mizigo na magari kati ya Bugorola-Ukara Wilaya ya Ukerewe Mkoa wa Mwanza na Chato-Nkome Wilaya ya Chato mkoani Geita.
Uzinduzi huo umefanyika mkoani Mwanza eneo la karakana ya Kampuni ya Songoro Marine Transport Boaty Ltd, inayojenga vivuko hivyo ambapo viongozi mbalimbali wa Serikali kutoka Chato na Ukerewe walihudhuria hafla hiyo.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme (Temesa), Mhandisi Japhet Masele alisema Serikali imeamua kujenga vivuko hivyo kutokana na kuwapo na mahitaji makubwa hususani Ukerewe ambapo hivi karibuni kulitokea ajali eneo la Bugorola na kusababisha vifo vya watu.
Mhandisi Masele alisema kivuko cha Bugorola-Ukara kitajengwa na Kampuni ya Songoro Marine Transport Boaty Ltd kwa Sh. bilioni 4.2 bila kuwapo na Ongezeko la Thamani (VAT) huko kile cha Chato- Nkome kitagharimu Sh bilioni 3.1.
“Vivuko vyote vitagharimu Sh bilioni 7.3 ambazo zote zitatolewa na Serikali, kwa mujibu wa mikataba tuliyoingia na kampuni hii ni kwamba vivuko hivi vitajengwa kwa miezi 10 tu, hivyo tunamuomba mzabuni wetu ambaye ni mzawa akamilishe kazi hii kwa wakati.
“Kivuko cha Bugorola-Ukara kitakuwa na na vipimo vya urefu wa mita 39, upana mita 10 na kitaelea ndani ya maji kati ya mita 0-7 hadi 1.0, pia kitakuwa na uwezo wa kubeba tani 100 yaani abairia 300, magari 10 na mizigo, vile vile kivuko cha Chato-Nkome kitakuwa na uwezo wa kubeba abiria 200, magari 10 na mizigo.
“Vivuko hivi vitafungwa injini mbili na vitaendeshwa na mifumo miwili ya usukani ambapo moja itakuwa ni ya dharula, kama mtakumbuka nimewaambia tunataka kuimarisha usalama majini na usafiri wa uhakika ndiyo maana vinajengwa kwa mabati maalum ya daraja la kwanza ‘grade A marine’ hivyo natarajia Aprili, 2020 tutakabidhiwa,’alisema.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Songoro Marine Transport Boaty Ltd,Major Songoro aliipongeza Serikali kwa kumwamini na kumpa zabuni za kujenga vivuko hivyo huku akiahidi kuvikabidhi Februari na si kama mkataba unavyoelekeza Aprili, 2020.
“Kutokana na Serikali kuwa na imani na mimi, naahidi kwamba vivuko hivi navikabidhi Februari, 2020 na si kama mkataba unavyosema nikabidhi Aprili, kama mnavyoona wafanyakazi wameanza kazi rasmi na wana utayari wa kufanya kazi, binafsi naogopa kusema mambo mengi bali nataka vitendo ndio viongee zaidi,”alisema.
Kwa upande wa Mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhandisi Warioba Sanya amesema ujenzi wa vivuko hivyo ni utekelezaji wa ahadi ya Rais Mhe.Dkt. John Magufuli ya kutaka kuboresha na kuimarisha usalama wa abiria na vyombo vya majini ndani ya Ziwa Viktoria.
“Hapa kinachotekelezwa ni ahadi ya Rais wetu na ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), hatutaki yale yalitokea Bugorola yatokee tena, sote tunajua mahitaji yaliyopo pale Bugorola ingawa kuna kivuko cha MV. Sabasaba kinafanya kazi pale.
“Kama Serikali tumekusudia kuwawezesha wakandarasi wa ndani ili fedha hizo ziweze kubaki hapa hapa, pia Mwanza ipo katika mkakati maalumu wa kuwa kituo cha uchumi katika Nchi za Afrika Mashariki ndiyo maana tunataka kampuni hii iwezeshwe na kuwa mahiri kwa ajili ya kujenga meli kubwa hapa hapa Mwanza, hivyo tunawaomba viongozi wa kampuni hii wajitahidi sana katika kazi,”alisema.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.