Shamba la Taifa la Mifugo Mabuki liwekewe miundombinu ya visima ili kuwa na Malisho bora: RAS Mwanza
Leo Januari 4, 2024 Katibu Tawal Mkoa wa Mwanza Balandya Elikana amefanya mazungumzo mafupi Ofisini kwake na Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Prof. Daniel Mushi ambapo ametoa rai kwa Wizara hiyo kuweka miundombinu ya visima vya Maji kwenye Shamba la Mabuki ili uoteshaji wa Malisho uwe endelevu.
Balandya amesema mradi huo uliopo Wilayani Misungwi ambao umewalenga vijana kujikwamua kiuchumi kwa kuwa wafugaji bora ni mzuri ila changamoto iliyopo ya uhaba wa maji unarudisha nyuma malengo yaliyokusudiwa na Wizara.
"Ndugu Naibu Katibu Mkuu, wakati wa kiangazi suala la Malisho linakuwa tatizo kutokana na uhaba wa malisho na kufanya mifugo kushuka ubora wake na kushindwa kupata soko",amefafanua Mtendaji huyo wa Mkoa wakati wa mazungumzo mafupi na Mtendaji huyo wa Wizara sekta ya mifugo.
Balandya amebainisha kuwa Ofisi yake hivi sasa ipo mbioni kukamilisha Maduka maalum ya nyama yapatayo matano ili kuwahakikishia soko vijana hao wa Mabuki walipo kwenye Mradi wa Jenga kesho iliyo bora (BBT).
Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu Prof. Mushi amesema changamoto zilizopo katika shanba hilo Wizara inazitambua likiwamo tatizo sugu la uvamizi kutoka kwa wananchi na sasa wapo mbioni kuweka ulinzi wa kudumu kutoka Suma JKT.
"Nakuhakikishia Ras tutaanza kuwaondoa wavamizi wote hivi karibuni na kuweka ulinzi wa kudumu,tutaboresha nyumba za kulala za vijana wanaendelea kuingia kwa awamu kupata mafunzo kwenye vituo atamizi,na pia suala la visima litapatiwa ufumbuzi muda siyo mrefu," Naibu Katibu mkuu.
Ameongeza kuwa mradi huo ni jicho la Mhe Rais Samia ambaye ndoto yake ni kuona kundi la vijana wanaokosa ajira wanakombolewa na mradi huo ambao umewekewa mikakati yenye tija.
"Upo mfuko maalum ulio na Shs bilioni 130 ambao utaingizwa kwenye baadhi ya Taasisi za kibenki ili kuwakopeaha vijana hao mara baada ya kupata mafunzo hayo ya unenepeshaji mifugo lengo likiwa wawe wafugaji bora na siyo wachungaji",amesisitiza Naibu Katibu mkuu huyo.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.