Shirikisho la Walimu Makada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Mwanza linatarajia kufanya shughuli za kijamii katika kuadhimisha mwaka mmoja wa Shirikisho hilo tangu kuanzishwa kwake.
Akizungumza kwa niaba ya mwenyekiti Jackson Kadutu, Katibu wa Shirikisho Mwalimu David Sulube amesema katika kuunga mkono juhudi zinazofanywa na Serikali ya awamu ya sita wameamua kutoa Msaada kwa Mama na Mtoto kwenye Hospitali ya Buzuruga wenye thamani ya Tshs. Milioni 2 siku ya jumamosi ya tarehe 08 Oktoba, 2022.
Aidha, mwalimu Sulube amesema kuwa katika maadhimisho hayo wanatarajia pia kupanda Miti elfu kumi kwenye wilaya zote za Mkoa huo ambapo uzinduzi Rasmi wa shughuli hiyo utafanywa katika shule ya Sekondari Lugeye iliyopo wilayani Magu siku ya ijumaa ya tarehe 07, 2022.
Amesema, kwenye siku hiyohiyo ya ijumaa kutakuwepo na ugawaji wa taulo za kike zenye thamani ya Tshs. Milioni mbili na laki tano kwa watoto 300 wa kidato cha tano na sita katika shule hiyo kwa awamu ya kwanza lakini pia zitagawiwa taulo hizo kwa watoto wenye mahitaji maalumu katika shule ya Sekondari Buhongwa.
"Siku ya jumamosi shirikisho tutakuwa na Shughuli nyingine muhimu sana ya kijamii ya uchangiaji wa damu na utoaji wa misaada kwa mama na Mtoto," amefafanua Mwalimu Kaligiwa.
Shirikisho la Walimu wa Chama Cha Mapinduzi limeipongeza Serikali kwa kutekeleza Ilani ya CCM ibara ya 84 inayotaka kuboreshwa kwa huduma za afya hususani Mama na Mtoto kwani baada ya kuboresha vifaa tiba kwenye Hospitali ya Buhongwa kumekua na ongezeko la wamama wanaojifungua hadi 600 kwa mwezi kutoka 200 siku za nyuma.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.