Somo la Michezo lifundishwe Shuleni ,Vyuoni – Majaliwa
Waziri Mkuu Mhe.Kassim Majaliwa amesema kuwa somo la elimu ya Michezo linatakiwa kufundishwa kuanzia shule za msingi,sekondari hadi vyuo vikuu ili kukuza viwango vya michezo na vipaji kwa vijana Tanzania.
Mhe. Majaliwa alisema hayo Mkoani Mwanza katika uwanja wa CCM Kirumba, wakati akifungua rasmi mashindano ya shule za Sekondari na msingi( UMISSETA na UMITASHUMTA) Taifa kutoka Mikoa 26 ya Tanzania bara na Mikoa 2 kutoka Unguja na Pemba Zanzibar.
“Kauli mbiu yetu mwaka huu katika Mashindano ya umiseta na umishumitani,Michezo, Sanaa na Taaluma ni Msingi wa maendeleo ya wanafunzi katika Taifa letu,”alisema Majaliwa.
Mhe. Majaliwa aliongeza kuwa Serikali imeweka kipaumbele katika suala la michezo mashuleni,huku akizitaka Wizara ya Elimu,Sayansi na Teknolojia, kushirikiana na Wizara ya Habari,Utamaduni Sanaa na Michezo kuhakikisha somo la michezo linafundishwa kuanzia shule za msingi, Sekondari hadi vyuo vikuu ikiwa lengo ni kukuza kiwango cha michezo Nchini na vipaji kwa vijana.
Aliziagiza Halmashauri zote Nchini kuhakikisha zinatenga bajeti kwa ajili ya michezo katika shule za msingi na Sekondari na kuwapa fursa walimu wenye uwezo wa kufundisha michezo shuleni ,badala ya kuwapa bora walimu kufundisha somo hilo.
Waziri Majaliwa amewaonya maofisa Elimu na walimu wa michezo mikoani kutohujumu mashindano hayo kwa kuingiza watu wasio wanafunzi kushiriki ambao ni ’’ Mamluki”kuwa wakigundulika wamefanya hivyo hatua kali dhidi yao zitachukuliwa na Serikali.
Awali naibu Waziri Ofisi ya Rais Tamisemi Dkt. Leonard Akwilapo amesema kuwa mashindano hayo yamelenga kuibua wanamichezo nchini kutengeneza ajira ambapo tayari baadhi ya vijana wamefanikiwa kutokana na michezo.
Mhe. Akwilapo amesema mfano wa wachezaji wa mpira wa miguu ambao wamefikia kiwango bora waliotokana na michezo shuleni ambao ni Edibily Lunyamila aliyewahi kuchezea timu ya Yanga, Shiza Kichuya ambaye ni mchezaji nyota wa Simba na Mbwana Samatta ambaye kwa sasa yuko nchini Ubeligiji akichezea timu Genk iliyopo ya ligi kuu .
Naye Mwalikishi wa kampuni ya COCA COLA ambao ni wadhamini wa mashindano hayo ,David Kalamagi wameahidi kuendelea kudhamini mashindano hayo na kufanya maboresho kwenye baadhi ya mapungufu yaliyojitokeza wakati wa mashindano hayo.
Mashindano hayo ya Umiseta na Umitashumita yameshirikisha jumla ya wanafunzi 6480 kutoka mikoa yote ya Tanzania bara na visiwani.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.