UFUGAJI WA KISASA WA SAMAKI UTAONGEZA TIJA KWA NCHI ZA AFRIKA MASHARIKI :NAIBU WAZIRI
Mkutano wa tatu wa ukuzaji viumbe maji Afrika Mashariki umefunguliwa rasmi leo Agosti 13, 2024 Jijini Mwanza na rai imetolewa ya kutolewa kwa elimu ya ufungaji wa kisasa wa samaki kwa njia ya vizimba.
Akifungua mkutano huo, Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe.Alexander Mnyeti amesema uvuaji holela umepitwa na wakati na umesababisha samaki wengi kupotea wakiwemo Ningu na Gobogobo.
Mnyeti amebainisha kuwa licha ya ziwa hilo sehemu kubwa kuwa Tanzania lakini bado hatujalitumia vizuri kulinganisha na wenzetu wa nchi jirani kama Uganda.
"Huku kwetu tuna jumla ya vizimba 168 hivi kwenye ziwa Victoria na Tanganyika lakini Uganda wao wana vizimba zaidi ya 2000, hapa tunaona bado tunahitaji mkazo wa kuelimishana", Mhe. Mnyeti.
Amesema, Serikali imeweka mazingira mazuri katika sekta ya uvuvi kwa kutoa fursa za mikopo bila riba kutoka benki ya TADB lengo likiwa ni kufanya shughuli hiyo kwa tija.
Amezitaka pia taasisi zinazojihusisha na maendeleo ya ziwa Victoria kuzidi kubuni mikakati ya kuwalinda viumbe maji kwa kulipumzisha ziwa hilo na shughuli za uvuvi.
Akitoa salamu fupi za Mkoa wa Mwanza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa, Mkuu wa Wilaya ya Ilemela Mhe. Hassan Masalla ameishukuru Serikali ya Rais Samia kwa kuzidi kuiboresha sekta ya uvuvi na ajira kwa ujumla.
"Zaidi ya Tshs bilioni tano zimeletwa Mwanza, boti 26 za kisasa pamoja na vizimba 16, hii imechangia kuongeza tija katika sekta hiyo", ameeleza Mhe.Masalla.
Jumla ya Mataifa 18 yanashiriki mkutano huo zikiwemo Uganda, Kenya, Malawi, Zambia, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo pamoja na Nigeria.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.