Meneja wa Wakala wa Barabara Mkoa (TANROAD) Mhandisi Rubirya Marwa anasema ofisi yake imeendelea kutekeleza agizo la ilani la ukarabati wa barabara zote unaoendelea sanjari na ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami ambao umekwishaanza katika barabara kuu na zile za mikoa.
Anazitaja baadhi ya kazi zilizofanyika kuwa ni pamoja na mateng’enezo ya dharula katika barabara za Mabuki-Jojiro, Nyamazugo-Bukokwa, Nyamilama-Lubala kwa gharama ya shilingi Milioni 872.
“Kazi zinazoendelea ni pamoja na ujenzi wa madaraja ya Nyancheche na Tunyenye kwenye barabara ya Sengerema-Ngoma, Nyakato (Veta)-Buswelu-Mhonze kwa kiwango cha lami,” anasema.
Kwa upande wa utekelezaji wa shughuli za Mfuko wa Maendeleo, anasema jumla ya shilingi Milioni 2,533.065 zimepokelewa kutoka kwenye Mfuko wa barabara na zimetekeleza kazi ya ukarabati wa uwanja wa ndege, upanuzi wa barabara ya Makongoro-Uwanja Ndege na upanuzi wa daraja la Sukuma.
Kwa upande wa utekelezaji wa miradi ya maendeleo,anasema kazi zinazoendelea kufanyika kwa sasa ni pamoja na usanifu wa kina kwenye barabara za Magu –Ngudu –Hungumalwa(Km.70); barabara ya Sengerema –Nyehunge –Kahunda (Km. 80) na barabara ya Mwanza –Shinyanga (Mpakani).
Usafirishaji majini
Mkoa wa Mwanza ni mongoni mwa mikoa ya kanda ya ziwa iliyokuwa inakabiliana na changamoto ya usafiri wa majini kutokana na baadhi ya meli zilizokuwa zikitoa huduma.
Lakini kutokana na uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali ya awamu tano, Serikali imetenga mabilioni ya fedha kwa ajili ya ujenzi wa meli mpya na ukarabati wa meli nyingine.
Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Huduma za Meli (MSCL) Erick Hamissi anaishukuru Serikali kwa kutoa fedha ambazo zimeboresa huduma za usafiri katika ziwa Victoria, ambapo Serikali kupitia MSCL inatekeleza miradi mikubwa mitatu.
Anaitaja miradi hiyo kuwa ni ujenzi wa meli mpya yenye uwezo wa kupakia abiria 1,200 na tani 400 ya mizigo unaotekelezwa kwa gharama ya zaidi ya Sh89 bilioni.
Kujengwa kwa meli hii siyo tu kutarahisisha usafiri wa majini kati ya miji ya Bukoba na Mwanza, bali pia itachochea ukuaji wa uchumi katika mikoa ya Kagera na Mwanza ambako kwa kipindi kirefu hakuna usafiri wa uhakika wa majini.
Meli hii mpya inajengwa zaidi ya miaka 20 tangu kupinduka na kuzama kwa meli ya Mv Bukoba katika ajali iliyotokea Mei, 1996.
Yusuf Mugisha, mkazi wa mtaa wa Nyabulogoya jijini Mwanza anasema ujio wa meli hiyo utashusha bei ya bidhaa za chakula, hasa ndizi kutoka mkoani Kegera ambayo kwa sasa inasafirishwa kwa njia ya barabara.
“Hivi sasa mkungu mmoja wa ndizi ya Bukoba unauzwa kati ya Sh15, 000 hadi Sh25,000 kutegemeana na ukubwa na ubora. Bei hii itashuka baada ya meli kukamilika kwa sababu usafirishaji kwa njia ya maji ni rahisi kulinganisha na barabara inayotumika kwa sasa,” anasema Mugisha
Serikali pia inajenga chelezo itakayotumika kujengea meli na vyombo vingine vya usafirishaji majini kwa gharama ya Sh36 bilioni.
Ukarabati wa meli za Mv Victoria, Mv Clarias na Mv Butiama pia zinakarabatiwa kwa gharama ya zaidi ya Sh27 bilioni.
Mradi wa ujenzi wa meli mpya ulioanza rasmi mwezi Januari mwaka huu, unatekelezwa na Kampuni ya Gas Entec na Kang Nam Corporation zote kutoka Korea kwa kushirikiana na SUMA JKT na kazi hiyo imekamilika kwa zaidi ya asilimia 30.
Erick anasema ujenzi wa chelezo ulioanza rasmi mwezi Machi mwaka huu ukitekelezwa na Wakandarasi wawili STX Engine Co Ltd na SAEKYUNG Construction Ltd kutoka Korea Kusini kwa gharama ya umefikia asilimia 34.
Kwa upande wa ukarabati wa meli za Mv Victoria, Clarias na Butiama, unafanywa na Kampuni ya KTMI kutoka Korea Kusini kwa kushirikiana na Yuko Enterprises EA ya Tanzania utekelezaji umefikia asilimia 36 na kazi hiyo ya ukarabati inatarajia kukamilika mwezi Machi mwakani.
“Ujenzi wa meli mpya na ukarabati wa meli hizi tatu ambazo zikikamilika zitaboresha sana maisha ya watu wa kanda ya ziwa, hii ni ahadi ya Mheshimiwa Rais tunamshukuru sana kwa kutoa fedha kwa ajili ya miradi hii mikubwa kwa ukanda wa ziwa Victoria,” anaeleza.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.