*Usalama wa Wananchi ni Kipaumbele changu- RC MAKALLA*
*Aomba Ushirikiano kufanikisha Maendeleo mkoa wa Mwanza*
*Atangaza ratiba ya Usikilizaji Kero za wananchi Jimbo kwa Jimbo*
*Awataka watumishi kujibu kero za wananchi kwa wakati*
*Aagiza uimarishwaji wa Mapato ya ndani na Idara ya Ardhi isimame imara kutatua kero*
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Amos Makalla amewataka viongozi wa wilaya ya Ilemela kusimamia masuala ya Usalama wa jamii ili wananchi wawe huru kufanya kazi za kujitafutia maendeleo.
CPA Makalla amebainisha hayo mchana wa leo Mei 31, 2023 kwenye Ukumbi wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela alipofika kujitambulisha kufuatia kuhamishiwa kwake na Mhe. Rais Mkoani Mwanza mapema mwezi huu.
"Watu wakikosa usalama watakosa amani ya kufanya mambo ya Maendeleo hivyo lazima tukumbushane umuhimu wa kuwa na amani kwenye maeneo yetu ili kuleta tumaini kwa wananchi kuwa wapo huru kujitafutia kipato." Amesema Makalla.
Aidha, Mhe. Makalla amesisitiza nidhamu ya kazi kwa watumishi ili wananchi wapate huduma bora na kuiamini serikali yao na kuondoa hofu na dukuduku kwa watumishi wa umma.
"Mkiwahudumia vyema mwananchi wataipenda Serikali na kinyume chake wataichukia hivyo tuepushe migogoro na migongano kwenye maeneo yenu ya kutolea huduma." CPA Makalla.
Vilevile, ameiagiza Halmashauri hiyo kusimamia kwa dhati ukusanyaji wa mapato ya ndani ili wawe na rasilimali za kutosha kutekeleza miradi mbalimbali kwa jamii na kwamba wote kwa pamoja ni lazima wadhibiti Mapato ya ndani na wajiwekee utaratibu wa kujibu Hoja za Ukaguzi kwa wakati.
"Hakikisheni fedha zote zinazokusanywa zinakwenda Benki ili tuweze kujihakikishia ukusanyaji mzuri na kuwahudumia wananchi kwa kutekeleza miradi mbalimbali na wabadhirifu wa fedha wajue kabisa kuwa tunawafuatilia" Amesisitiza.
Aidha, amewaagiza viongozi na watumishi kujibu kero za wananchi kwa wakati na kutosubiri ofisini bali wawafuate kwenye makazi yao na kwamba atafanya ziara ya kusikiliza kero za wananchi kwenye kila wilaya na atawapima wetakaobainika kuwa na kero nyingi.
"Nimekuja kuwasalimia na kujitambulisha kwenu hivyo naombeni sana ushirikiano wenu Viongozi, waheshimiwa Madiwani na watendaji wote tufanye kazi kwa pamoja ili kwenye mafanikio tuwe pamoja na kwenye Changamoto tuwe pamoja pia, hodi Mwanza." Mhe. Makalla.
Mkuu wa Wilaya ya Ilemela Mhe. Hassan Masala amesema wilaya hiyo unaendelea kuboresha mazingira kwa kuwaletea huduma bora za Miundombinu, Elimu na Afya na kwamba makundi yote yanawezeshwa vema kupitia idara ya Maendeleo ya Jamii.
Aidha, amebainisha kuwa kwa Mwaka wa fedha inayoendelelea (2022/23) Halmashauri ya Wilaya ya Ilemela imekadiria kukusanya Shilingi Bilioni 13 na hadi sasa wamekusanya zaidi ya bilioni 14 ambayo ni sawa na asilimia 109 na wanaendelea kutekeleza Miradi yenye thamani ya Bilioni 18.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.