VYAMA VYA USHIRIKA VYATAKIWA KUTUMIA MIFUMO YA TEHAMA
Naibu Waziri wa Kilimo Mhe. David Silinde (MB) amewataka viongozi wa vyama vya ushirika kutumia mifumo ya kisasa ya Tehama na kuacha kufanya kazi kwa kutumia mifumo ya zamani ili waweze kutoa huduma bora katika vyama.
Amesema hayo leo Oktoba 21, 2024 wakati akifungua maadhimisho ya siku ya kimataifa ya ushirika wa akiba na mikopo mwaka 2024 yanayofanyika Kitaifa Mkoani Mwanza katika viwanja vya Mirongo Wilaya ya Nyamagana.
Aidha Mhe. Silinde amesema ili kuweza kuleta maendeleo katika vyama vya ushirika viongozi wa vyama hivyo wanatakiwa kufanyakazi kwa kufuata sheria na miongozo.
" Viongozi waendelee kusimamia ushirika kwa kufuata misingi, kanuni, sheria na miongozo kwa ajili ya kuleta maendeleo"amesema Mhe. Silinde.
Kadhalika Kaimu Katibu Tawala Msaidizi Uchumi na Uzalishaji Mkoa wa Mwanza Bwana Peter Kasele kwa niaba ya Katibu Tawala amewataka wananchi kutumia fursa ya maadhimisho ya siku ya kimataifa ya ushirika wa akiba na mikopo katika kujipatia elimu ya masuala ya fedha.
Sambamba na hayo bwana Kasele amesema kuwa Serikali ya Mkoa inatambua umuhimu na mchango wa vyama vya ushirika katika kuleta maendeleo kwa watumishi pamoja na wananchi.
Naye MwenyeKiti wa Bodi ya chama kikuu cha Ushirika wa Akiba na mikopo Tanzania SCCULT Mwl. Aziza Mshana amesema chama hicho kinashukuru kwa mchango wa Serikali katika kuthamini mchango wa ushirika wa akiba na mikopo katika kukuza uchumi.
Maadhimisho hayo yanafanyika kwa muda wa siku 5 kuanzia Oktoba 20, 2024 mpaka Oktoba 24, 2024 yenye kauli mbiu ya "Ulimwengu Mmoja kupitia Ushirika wa Kifedha" yanaadhimishwa kwa mara ya 76 Duniani na 15 kwa nchi ya Tanzania tangu kuanzishwa kwake.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.