Wakazi wa Kijiji cha Chifunfu kilichopo wilayani Sengerema Mkoa wa Mwanza wamemuomba Waziri Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mhe. Seleman Jaffo kufika katika wilaya hiyo ili kuona namna watoto wanavyoteseka kutembea umbali wa kilomita 19 kwenda sekondari ya Chifunfu unaosababisha mimba nyingi kwa wasichana.
Ombi hilo lilitoa juzi katika mkutano wa hadhara uliofanyika eneo ilipojengwa Shule mpya ya Sekondari Bugumbisiko ambayo haijaezekwa vyumba sita vya madarasa.
Wakazi hao ambao ni, Janeth Japhet, Simeo Lubinza, Mathias Sweka walisema tangu diwani huyo achaguliwe amekuwa si kiongozi wa kutatua changamoto zao bali mambo yake binafsi kitendo ambacho kinasababisha watoto wao kupata mimba na kukatisha masomo hivyo kwa pamoja hawamtambui kama diwani wao.
“licha ya kujitolea kujenga shule nyingine ya sekondari ya Bugumbisiko imeshindwa kuezekwa na halmashauri ya Wilaya ya hiyo kwakuwa Diwani wa kata ya Chifunfu, Robert Madaha ndiyo anakwamisha jitihada zetu kutokana na itikadi za siasa”alisema Mathias Sweka
Vicent Magembe ambaye ni mjumbe wa serikali ya kijiji alisema diwani huyo hana nia nzuri na shule hiyo ambapo amekuwa akiweka vikwazo ngazi ya wilaya ili shule hiyo isiezekwe, pia alidai kuwa taarifa za sekondari ya Bugumbisiko amekuwa akizificha na kutojadiliwa kwenye baraza.
Alisema ndani ya kijiji hicho, watendaji wamekuwa wakibadilishwa mara kwa mara pale wanapoonekana kutomuunga ajenda zake, hivyo aliwataka wananchi kuwa na msimamo dhidi ya wakwamishaji maendeleo yao.
Akisoma taarifa za kamati ya ujenzi wa sekonadari ya Bugumbisiko, Katibu wa kamati hiyo, Fredick Nyamwanda alisema wananchi waliamua kuanzisha ujenzi wa shule hiyo baada ya shule ya kata iliyopo sasa kujengwa mbali na kijiji hicho ambapo watoto hutembea kilimita 19 ili kuifika ambapo wengi hushindwa kumaliza masomo kutokana na mimba zinazotokana na vishawishi wanavyopata njiani.
Alisema kutokana na adha hiyo, wananchi wa vitongoji vitatu kati ya tisa, vya Kijiweni, Mulumo na Luchanga waliamua kuanzisha ujenzi huo ambao vyumba sita vya madarasa vimekamilika huku nyumba ya mwalimu, maabara, jengo la utawala na ujenzi shimo la choo ukiwa katika hatua za mwisho kukamilika.
“Mpaka sasa ujenzi ulipofikia tumetumia sh. milioni 29.7 lakini kutokana na uongozi wa kijiji na kata kutokuwa karibu, kamati imepata wakati mgumu kupata pesa za kumalizia kutokana na kauli zinazotolewa na viongozi wetu, kwanza ujenzi huu umeingiliwa na siasa jambao ambalo limekatisha tamaa wananchi na wadau kutochangia,”alisema
Hata hivyo watendaji wa kata na vijiji walimtetea diwani huyo lakini zomea zomea ilizidi ambapo waliamua kukaa kimya na kumuomba diwani azungumze na wananchi wake.
Baadhi ya mabango yaliyokuwa yakionyweshwa mbele ya diwani huyo yalisomeka , Mheshimiwa Rais Magufuli umbali wa shule ndio chanzo cha mimba Chifunfu, ‘Waziri Seleman Jaffo tuunge mkono kwani diwani wetu hajachangia hata 100 na shule hataki, tunakuomba ututembelee kwetu Chifunfu’.Bango lingine lilisomeka kwamba ‘Rais wetu tunakuunga mkono kwa asilimia 100, tuangalie elimu ndio msingi wa maendeleo, hapa kazi tu’.
Kwa upande wa diwani, Madaha alisema si kweli anakwamisha ujenzi huo kwani amekuwa akijitahidi kumshawishi Mkurugenzi wa Sengerema ili kuwaezekea madarasa hayo na hatimaye shule iweze kusajiliwa na kuanza masomo mwakani.
“Jamani binafsi nasikitika sana juu ya malalamiko yenu na uamuzi wenu wa kuniita mchawi wa maendeleo yenu, najua tatizo ni siasa mnazichanganya na shughuli za maendeleo, kwanza mngejua ninavyopambana juu ya shule hii msingekuwa mnanisema vibaya hivi, naombeni muache masuala ya mitaani ili tujenge shule hii”alisema Madaha
Aliongeza, “Kwanza niwahakikishie hadi sasa bajeti ya kuezeka madarasa haya imetengwa katika bajeti inayoanza Julai Mosi mwaka huu, hivyo niwaomba wote tuwe wavumilivu”
MWISHO
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.