Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe.John Mongella amewataka wafanyabiashara wadogo kutumia fursa ya kujisajili na kutambuliwa ili kuweza kulipa kodi itakayosaidia kujenga uchumi wa nchi ili nao waweze kukopesheka.
Mhe. Mongella ameyasema hayo wakati wa wazoezi la uzinduzi wa utoaji wa vitambulisho kwa wafanyabiashara wadogo wadogo (wamachinga) Mkoani humo, ili waweze kutimiza wajibu wao kwa mujibu wa sheria na kuchangia pato la taifa.
“Kila mmoja wenu anayefanya biashara ndogondogo ana wajibu kufanya hivyo isipokuwa kwa walio katika sekta rasmi ya biashara na kwa yoyote ambaye hata jisajili katika mfumo huo hataruhusiwa kufanya biashara kiholela”,alisema Mongella.
Naye Kamisha Mkuu Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Charles Kichere alisema tayari imevitambua vikundi 130 jijini mwanza ambavyo wanachama wake ambao ni wafanyabiashara wadogo wadogo wanatarajiwa kupatiwa vitambulisho.
Aidha, Kichere aliongeza kuwa jukumu kubwa ni kukusanya mapato na kutoa elimu ya ulipaji kodi, na zoezi hili la kutoa vitambulisho maalumu kwa machinga na kuendelea kulipa kodi kwa hiari, zoezi hili ni endelevu na mwaka huu wa fedha umeweka marekebisho madogo madogo ya kuwatambua machinga kwa kushirikiana na Nida, Rita na uhamiaji namba ya mlipa kodi na kitambulisho cha kitaifa.
Kwa upande wake Naibu Kamishina kodi za ndani ufundi Michael Muhoja alisema tangu kuanza kwa zoezi hilo linafanyika nchi nzima na kwa Mkoa wa Mwanza wanatarajia kusajili vikundi 130,hadi sasa wameshatambua vikundi 37 vyenye jumla ya wafanyakazi 1,100 ambapo kwa uwakilishi wa siku hii ya uzinduzi wametoa vitambulisho 32.
Naye Said Tembo ambaye ni Mwenyekiti wa wamachinga Mkoani Mwanza amesema wanamshukuru Mhe. Rais Dkt. John Magufuli kwa kuthamini juhudi zao na kuagiza wapatiwe vitambulisho ili waweze kutoa mchango wao kwenye ujenzi wa uchumi wa Taifa kwa kulipa kodi.
" Zoezi hilo liharakishwe ili wamachinga wote nchini waanze kulipa kodi kwa ajili ya maendeleo ya Taifa" alisema Tembo.
Awali Mstahiki Meya wa Jiji la Mwanza James Bwire akihututia wafanya biashara hao alisema Mkoa unakadiriwa kuwa na zaidi ya wafanyabiashara wadogo elfu 15 ambao wakitambuliwa na kupatiwa vitambulisho itaiwezesha mamlaka ya mapato Tanzania(TRA)kupanua wigo wa kodi.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.