Siku chache baada ya Serikali mkoani Mwanza kuweka maazimio 14 kwa walimu wakuu, maofisa elimu wa kata na taaluma ili kuinua ufaulu kwa shule za msingi 2019/2020, imeanza kutekeleza kwa vitendo kwa wanafunzi wa darasa la saba wanaotarajia kufanya mtihani wa Taifa kati ya Septemba 11-12, mwaka huu.
Afisa Elimu Mkoa wa Mwanza, Michael Ligola kwa kushirikiana na maafisa elimu taaluma wa wilaya wamelazimika kutunga mtihani unaoelekeana na ule wa taifa na kuwakutanisha wanafunzi wa shule mbalimbali katika kituo kimoja ili kujipima.
Zoezi hilo limeanza ambapo baadhi ya shule kutoka Jiji la Mwanza na Ilemela zimekutanishwa pamoja katika Shule ya Msingi Nyanza na kupatiwa mtihani wa kujipima kwa kufuata muda na masharti yale yale yanayokuwepo katika mtihani wa kitaifa, ambapo shule itakayoifaulisha wanafunzi wengi itakabidhiwa fedha taslimu na mbuzi kwa ajili ya mahafali.
Akizungumza na waandishi wa habari kwa niaba ya Ligola, Afisa Elimu Taaluma Mkoa wa Mwanza, Longino Ludovick alisema lengo la Serikali ya mkoa ni kuhamasisha, kuboresha taaluma na kuwaandaa wanafunzi kuelekea mtihani wa taifa unaotarajia kufanyika Septemba 11 na 12, mwaka huu.
Amwongeza kuwa kwa wiki mbili zilizobaki wataendelea na zoezi hilo kwa shule mbalimbali ambapo changamoto zitakazokuwa zikionekana kwa wanafunzi zitatafutiwa majibu haraka kwa kipindi kilichobaki huku akianisha kwamba zawadi zitaanza kutolewa Agosti 30, mwaka huu.
“Leo kama unavyoshuhudia tumezikutanisha shule nne ambazo ni Butimba A na B, Bwiru na Gedeli ambazo zimetoka Ilemela na Jiji la Mwanza, hizi shule tumezikutanisha kwa sababu katika mtihani wa Mock zilifanya vizuri hivyo tunataka kuona ipi inaongoza, shule itakayofaulisha wanafunzi wengi watapata zawadi ya pesa na mbuzi kwa ajili ya kitoweo cha mahafali.
“Kwa wiki moja au mbili zilizobaki tutaendelea katika shule zingine na changamoto zitakazojitokeza tutazifanyia kazi haraka kabla ya mtihani wa taifa, mitihani hii imetungwa na jopo la maofisa elimu kutoka mkoani na wilayani ndio maana unatuona hapa tukishughulika katika kituo hiki cha Shule ya Msingi Nyanza".
Teleza Deus kutoka Shule ya Msingi Gedeli alisema maswali ya somo la Kiingereza waliyopatiwa ni marahisi ambapo aliahidi kupata 45 kwa 50 huku akifafanua kuwa walimu wao wamekuwa wakiwapa majaribio kila ijumaa, hivyo haoni shida kufaulu au shule yao kuibuka kidedea.
Naye Jovin Msiba kutoka Shule ya Msingi Bwiru alisema mtihani huo wa Kiingereza ni kawaida na maswali mengi aliyokutana nayo amefundishwa na walimu. Aliongeza kuwa walimu wao wamekuwa wakiwapatia majaribio ya kujipima kila wiki ambapo maswali mengi alikuwa anayajua.
Hata hivyo wanafunzi wengine, Julius William na Vailet Javis kutoka Butimba A na B walitamba kwamba shule yao itaibuka kidedea kwani maswali mengi wamejifunza.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.