Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda ametoa rai kwa wanahabari nchini kuzingatia sheria, kanuni na miongozo ya kitaaluma ili kufikisha habari za ukweli na kuepuka kusababisha migogoro kwenye jamii hususani katika kipindi cha uchaguzi Mkuu wa 2025.
Mhe. Mkuu wa Mkoa ametoa wito huo leo tarehe 07 Agosti, 2025 alipokua akifunga semina ya siku moja kwa makamanda wa Jeshi la polisi pamoja na waandishi wa habari na watangazaji kutoka mikoa ya kanda ya ziwa kuelekea uchaguzi Mkuu wa 2025.
Amesema kwa pamoja wanahabari na jeshi la polisi wanapaswa kuelimisha jamii kuhusu sera za wagombea, kuibua na kufuatilia ukiukwaji wa sheria, kuhamasisha ushiriki wa makundi maalum kama walemavu na wanawake pamoja na kupambana na taarifa potofu na propaganda.
"Serikali imefanya jitihada katika kurekebisha sheria na sera ili kuhakikisha uhuru wa vyombo vya habari unalindwa ikiwa ni pamoja na marekebisho ya Sheria ya Huduma za Habari Sura ya 229 yaliyofanyika kwa ushirikiano na wadau ambayo imesaidia kuongeza uwazi, ufanisi na imani ya umma kwa tasnia ya habari." Mhe. Mtanda.
Aidha, amebainisha kuwa maboresho hayo yamepelekea kukua kwa tasnia hiyo hata kuwa na zaidi ya Magazeti 375, Vituo vya redio 247, Televisheni 68, Vyombo vya habari mtandaoni 355 na Blogu 72 nchini ambazo si tu kwamba zimesaidia kutoa ajira bali pia kupata jukwaa pana la upashanaji habari.
Vilevile, ameipongeza Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania pamoja na Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari kwa kuandaa mafunzo hayo muhimu katika kipindi cha kuelekea Uchaguzi.
Naye, Kaimu Mkurugenzi wa Habari Maelezo Rodney Thadeus amesema mafunzo hayo yamelenga kukumbushana kanuni na wajibu wa makundi hayo katika kulinda amani kwa kujenga taswira chanya kwa kamii ili wananchi waweze kutumia fursa ya utaifa wao kushiriki katika uchaguzi mkuu.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.