Wananchi wa Kijiji cha Nyashingwe,Kata ya Chabula wilayani Magu, watengeneza madawati 54,kujenga vyumba viwili vya madarasa na ofisi ya walimu katika Shule ya Msingi ya kijiji hicho kwa nguvu zao ili kutatua changamoto ya wanafunzi kukaa chini na msongamano darasani.
Madawati hayo 54 yana thamani ya sh.milioni 2.7 huku maboma mawili ya vyumba vya madarasa hivyo ambayo bado hayajapauliwa yakigharimu zaidi ya sh.milioni 6.3.
Ofisa Mtendaji wa Kijiji hicho Devota Aloys alisema jana kwa Mkuu wa Wilaya ya Magu Salum Kalli, wakati akitoa taarifa ya miradi ya maendeleo inayotekelezwa kwa nguvu za wananchi kijijini humo.
Alisema kaya sita kila kitongoji za vitongoji vinne zimetengeneza dawati moja ambapo kitongoji cha Nyashigwe kimetengeneza madawati 9 kati ya 11,Kibambu 19 (bado 2), Nyamilomate 20 wanadaiwa moja 1 na Zuli 6 kati ya 8 hivyo madawati 54 kati ya 62 yamepatikana kulingana na mgawanyo wa kila kitongoji.
Aloys alisema madawati hayo yamepunguza uhitaji katika Shule hiyo ya Msingi Nyashigwe yenye wanafunzi 750 kutoka 146 hadi 84,ambapo ina madasara 7 kati ya 17 ili kukidhi mahitaji hivyo madarasa yaliyojengwa na wananchi yakiezekwa yatasaidia.
Pia alisema shule hiyo ina uhaba wa matundu 29 ya vyoo yaliyopo ni 6 kati ya 35 na kuiomba serikali iwasaidie kujenga vya kisasa ili kunusuru afya za wanafunzi na baada ya wananchi kujenga zahanati kwa nguvu zao na kukamilisha boma kwa sh. milioni 8 linahitaji kuezekwa.
Kwa upande wake Kalli alisema serikali lazima iunge mkono juhudi za wananchi na itaendelea kuboresha elimu baada ya kufuta ada kuanzia darsa la awali hadi sekondari kidato cha nne ili watoto wasome hasa wa kike na kwa heshima ya wananchi kwa kazi waliyoifanya atapeleka madawati 10 kwenye shule hiyo.
“Madawati haya yatawanufaisha watoto,elimu ni bure hivyo wazazi waacheni watoto wa kike muache tamaa ya mali, ni tunu katika taifa letu na hapa watatoka makamu wa rais, naibu spika,mawaziri na makatibu wakuu mbalimbali wanawake, kwanza ni waaminifu hawapindishi maneno kama wanaume,”alisema Kalli na kuwataka watoto wawaenzi wazazi na wananchi kwa kufaulu mitihani yao vizuri.
Pia alisema Aprili 30,atapaua na kuezeka vyumba vya madarasa vilivyojengwa na wananchi hao na atamwagiza Meneja wa Tanesco Magu aende kweye shule hiyo kupima nguzo zinazohitajika ili waunganishwe kwenye mradi wa umeme vijijini (REA).
Aidha baadhi ya wanafunzi wa shule hiyo,waliwashukuru wazazi na wananchi kwa kujitoa kwao na kuwajengea madarasa pamoja na kuwatengenezea madawati.
“Tunawashukuru wazazi kwa jitihada zao, wengi mavazi yalichafuka kwa tulikuwa tunakaa chini, pia tunamshukuru Rais John Magufuli kwa kutoa elimu bure,”alisema Bulala Simba.
Patrick Costantine yeye alisema madawati hayo yatakuwa kichochea cha kusoma kwa bidii ili wafaulu masomo na kutimiza ndoto zao huku Kado Safari akisema kuondolewa kwa changamoto ya kukaa chini wataongeza bidii ya kujifunza zaidi.
Mwalimu Mkuu wa shule hiyo Ishengoma Kabuche, alisema uhaba wa madawati na vyumba vya madarasa uliathiri utoaji wa taaluma na kushusha ufaulu, hivyo jitihada na mchango wa wananchi wa kuchonga madawati 54,ujenzi madarasa mawili na ofisi ya walimu kutaondoa msongamano wa wanafunzi darasani.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.