WANANCHI WA BUCHOSA WAMSHUKURU RAIS SAMIA KUWAJENGEA CHUO CHA UFUNDI STADI (VETA)
*RC Makalla awaagiza TANESCO na RUWASA kupeleka huduma kuharakisha ujenzi huo*
*Halmashauri ya Buchosa kupata Chuo cha Kwanza*
*Mkuu wa Mkoa awataka vijana kujiandaa na fursa za ajira kutokana na ufundi watakaopata chuoni hapo*
Leo Novemba 10, 2023 Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. CPA Amos Makalla amevuka milima na mabonde kufika kwenye Kijiji cha Kayenze kilicho pembezoni mwa Mji wa Nyegunge kwenye halmashauri ya Buchosa kukagua ujenzi wa Chuo cha Ufundi Stadi (VETA).
Akizungumza na wananchi kwenye eneo hilo la ujenzi Mhe. Mkuu wa Mkoa amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha zaidi ya Bilioni 3 kujenga chuo hicho ambapo amebainisha kuwa kitawajenga kiufundi katika fani mbalimbali vijana wa Buchosa na wilaya ya Sengerema kwa ujumla.
"Halmashauri ya Buchosa mmepata bahati sana, Rais Samia Suluhu Hassan anajenga vyuo kwenye halmashauri 63 kwa wakati mmoja ikiwemo na halmashauri yenu, nawapongeza sana kwa hili maana vijana wetu hapa watapata ujuzi kwenye fani mbalimbali ambapo itawasaidia kupata nafasi kwenye miradi ya ujenzi kama wa barabara" Makalla.
Makalla ametumia wasaa huo kuziagiza TANESCO na RUWASA kuhakikisha wanapeleka huduma za umeme na maji kwenye ujenzi huo ili kurahisisha shughuli zinazoendelea kwa kasi kwenye eneo hilo ambapo ndani ya wiki mbili tangia waanze ujenzi wamekwishafikisha asilimia 18 ya ujenzi.
"Umuhimu wa VETA hii ni mkubwa sana kwa vijana fani nyingi zitatolewa hapa kama umeme, mapishi, useremala, bomba na uashi hivyo itakua ni nafasi ya kijana kuamua asomee nini ili akajishughulishe mtaani kwenye kuinua uchumi wake." Amesisitiza Makalla.
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi wilaya ya Sengerema Mhe. Dominic Makoye amemshukuru Mkuu wa Mkoa wa kusimamia utekelezaji wa Ilani na ametoa wito kwa wataalam kuendelea kutoa ushirikiano kwenye kukamilisha mradi huo kwa manufaa ya vijana wa Buchosa.
Akizungumza kwa niaba ya wananchi, Diwani wa Kata ya Nyehunge Mhe. Dickens Kulwa amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa mradi huo ambao ameutaja kuwa unawasaidia wananchi kupata fedha kutokana na shughuli ndogondogo wanazofanya kwenye mradi huo.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.