Viongozi wa Wilaya ya Magu wametakiwa kuhakikisha kuwa wananchi wanajiandaa vema katika zoezi la sensa ya watu na Makazi itakayofanyika Agosti 23 2022, huku Elimu kuhusu Sensa imetakiwa kuendelea kutolewa maeneo mbalimbali ili ifikapo mwezi Agosti wananchi wote wawe wamepata taarifa.
Hayo yamebainishwa na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Mhe.Dkt.Stergomena Tax wakati akitoa salamu za mwenge wa Uhuru katika viwanja vya Kisasa mapema hii leo.
"Taarifa zote zitakazokusanywa wakati wa Sensa zitakuwa ni kwa malengo ya maendeleo ya Nchi na si vinginevyo niwaombe elimu iendelee kutolewa ili ifikapo Agosti 23 elimu iwe imefika hadi maeneo ya vijijini,"amesema Mhe. Tax.
Aidha, Mkuu wa Wilaya ya Magu Mhe.Salum Kalli awali akiwasilisha salamu za Wilaya ya Magu kwa Kiongozi wa mbio za mwenge wa Uhuru Ndugu Sahili Nyanzabara Geraruma amemtaka Kiongozi huyo kumfikishia Salamu za Shukurani Mhe.Rais kwa kuendelea kutuletea fedha za miradi mbalimbali ikiwemo Elimu, Afya,Maji na Miundombinu ya barabara.
Mhe.Kalli ameahidi usimamizi mzuri wa miradi yote na kusisitiza kuwa Mhe.Rais ana imani kubwa na viongozi aliowapa dhamana hivyo wasimuangushe.
"Ndugu Geraruma tupelekee salaam za Shukurani za wana Magu kwa Mhe.Rais kwamba sisi wana Magu tunashukuru sana kwa kuendelea kutuletea fedha za miradi mbalimbali ya maendeleo katika Wilaya yetu, tunaahidi kuendelea kusimamia vema miradi tunayopewa," amesema Mhe.Kalli.
Naye Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe.Marry Masanja amesema hatawavumilia watendaji kazi wasioendana na kasi ya Mhe.Rais. kwa kuwa Mhe. Rais analeta fedha nyingi sana kwa ajili ya maendeleo hivyo hatuna budi kusimamia kikamilifu.
Naye Mbunge wa Jimbo la Magu Mhe. Destery Kiswaga amewahimiza wananchi wote wa magu kushiriki kikamilifu zoezi la Sensa ili kuiwezesha Serikali kupanga maendeleo kwa kwa kuzingatia idadi ya watu.
Hata hivyo, Ziara ya Mwenge wa Uhuru imeingia katika siku ya tatu mkoani Mwanza katika Halmashauri ya Wilaya ya Magu ambapo Mwenge wa Uhuru
umezindua miradi 3,kukagua miradi 2 na kuweka jiwe la msingi mradi 1 yote ikiwa na thamani ya shilingi bilioni 1.02 ambapo kesho, Julai 15 itakabidhiwa Wilaya ya Ilemela na utakuwa umekamilisha kilomita 120 tokea ukimbizwe Wilaya ya Magu.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.