WATALII KUTOKA RS MWANZA WAOMBA KUWEPO NA MUENDELEZO ZIARA ZA NJE
Watumishi kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza ambao ni kundi la tatu kutembelea vivutio vya utalii wamepongeza uamuzi wa Uongozi wa Mkoa kwa kupitisha wazo la kuwapeleka kutalii Watumishi na kuomba kuja na mpango mkakati endelevu wa programu hiyo.
Watumishi hao waliopata fursa ya kutembelea Hifadhi ya Taifa ya Serengeti na Hifadhi ya Ngorongoro wameonesha kufurahia zaidi programu hiyo ambayo imelenga kuboresha na kuimarisha mahusiano, ari za kazi, umoja na mshikamano pamoja na uwajibikaji.
Akizungumza mara baada ya kutembelea hifadhi hizo Afisa Utumishi Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Bw. Credo Lugaila ambaye ndiye Kiongozi wa kundi hilo amesema kutembelea vivutio hivyo vimewapatia nafasi ya kufahamu rasilimali za Taifa, umuhimu wa rasilimali hizo na kuanzia hapo watakwenda kuwa mabalozi wazuri wa utalii wa ndani.
“Hata pale Ofisini kuna Idara zinazohusika na Utalii, mifugo na Maliasili hivyo ujio wetu hapa pia ni kuona kwa vitendo yale tunayoyatekeleza katika Ofisi zetu”.
Aidha Muuguzi Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Bi. Claudia Kaluli amesema yeye kama Mtumishi anayetoka idara ya afya kuna kitu kinaitwa afya ya akili ambapo ni pamoja na Mtumishi kupata walau muda wa kujifunza mambo mapya ambayo yatamjenga kifikra na kuchochea ari ya kazi pindi atakaporejea kazini.
“Mtumishi akiwa kwenye mawazo sana atashindwa kutekeleza vizuri kazi, hata sisi tukirudi hiyo kesho kutwa tutakuwa vizuri maana tutakuwa fresh kiakili”.
Kwa mfano hata kupitia picha tunazozisambaza kwenye mitandao ya kijamii marafiki zetu wamekuwa wakishangaa sana na kuona kuwa tunathaminiwa na kujaliwa na Viongozi wetu kwa kiasi kikubwa hivyo hali hii inatufanya tukirudi kazini tutimize wajibu wetu kwa kufanya kazi kwa bidii. Amesema Bw. Hassan Malupu Dereva kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa.
Ziara hiyo ya siku tatu imekuwa na manufaa makubwa kwa Watumishi hao ambao wamejivunia kuthaminiwa na Viongozi wao wa Mkoa, Mhe. Said Mtanda Mkuu wa Mkoa pamoja na Katibu Tawala Mkoa Bw. Balandya Elikana.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.