WATUMISHI RS MWANZA WAPIGWA MSASA ELIMU YA BIMA
Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) imeendesha kikao cha utoaji elimu ya Bima kwa Watumishi wa Serikali kuhusu uhamasishaji wa matumizi ya bidhaa za bima.
Akifungua kikao hicho mapema leo Machi 03, 2025 katika ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Katibu Tawala Mkoa wa Mwanza Bw. Balandya Elikana ametoa rai kwa Watumishi hao kuhakikisha wanakuwa makini katika kusikiliza elimu hiyo ili ikawe na manufaa kwao na kwa wale ambao hawajahudhuria.
Katibu Tawala amesema ni matarajio yake kuwa elimu hiyo itawasaidia na kuhakikisha wanakuwa mabalozi wa bima kwa jamii wanayoihudumia, na kusaidia katika urahisishaji wa upatikanaji wa huduma za bima kwa wananchi.
Aidha Bw. Balandya amesema kutokana na Sheria ya bima ya afya kwa wote ametumia jukwaa hilo pia kuwataka Watumishi na wadau kwenda kutoa elimu kwa wananchi juu ya umuhimu na faida za bima ili wananchi waweze kujitokeza kwa wingi katika kukata bima.
“Uelewa wa elimu ya bima ni msingi wa mafanikio ya utekelezaji wa bima ya afya kwa wote, niwatake muwe makini katika kusikiliza na kuelewa”.
Naye Kamishna wa Bima Tanzania Dkt. Baghayo Saqware ametoa rai kwa watumishi wa Mkoa wa Mwanza kuhakikisha kuwa mali na miradi mikubwa ya Serikali inakatiwa bima ili kupunguza hasara zinazoweza kutokea wakati wa majanga.
Aidha amesmea bima haimkingi mtu tu bali majanga mbalimbalo ambapo kwa sasa hata wale wakulima, wafugaji na wajasiriamali wadogo wadogo nao wanaweza kukinga bidhaa, mazao na mali zao.
“Bima za Kilimo, mifugo zipo lakini tunakosa watu kwa sababu hawana uelewa wa kutosha, elimu hawana, niwaombe mkatufikishie elimu hii ili waweze kukata bima hizo”.
TIRA wako Mkoani Mwanza wakilenga kuwaelimisha Watumishi kuhusu fursa zilizopo katika sekta ya bima, ikiwa ni pamoja na kuwa mawakala wa bima na utekelezaji wa Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.