Naibu Waziri wa Afya, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Dkt. Faustine Ndugulile ameipongeza Hospitali ya Mkoa wa Mwanza Sekou Toure kwa kutenga dirisha la matibabu kwa wazee ili kupata huduma ya Afya na kuwataka waweke utaratibu mzuri kwa Afisa ustawi wa jamii ili apatikane maeneo ya huduma kwa ajili ya kutoa vibali vya huduma bure kwa wazee.
Dkt.Ndugulile ameyasema hayo alipotembelea Hospitali ya Mkoa wa Mwanza Sekou Toure na kujionea jinsi huduma zinavyotolewa kwa kuongea na wagonjwa na kupata maoni yao juu ya huduma hizo, kwani ameridhishwa kuona kuwa wagojwa wengi waliofika kupata huduma wameridhishwa na huduma zinazotolewa kwa wakati na ubora wa huduma hizo.
“Muweke utaratibu kuhakikisha wazee wanaokuja hawazunguki huku na kule kwenda kumtafuta Afisa ustawi wa jamii kwa ajili ya kuwaandikia vibali vya huduma bure,hakikisheni Afisa Ustawi anakuwepo hapa hapa ili wazee wasikae muda mrefu hospitalini na wapate huduma staiki,” alisema Ndugulile.
Naye Mganga Mkuu wa Mkoa Dkt.Rutachunzibwa Thomas, awali akitoa hotuba ya Mkoa kwa mgeni rasmi amesema kuongezeka kwa vituo vya afya vyenye nyota tatu kutoka kituo kimoja mwaka 2015 hadi vituo 116 mwaka huu, na kupungua kwa vituo vyenye nyota ziro ambavyo vilikuwa 151 mwaka 2015 kufikia vituo saba mwaka huu kumeimarisha zaidi huduma za Afya Mkoa wa Mwanza.
“Huduma zimeimarishwa zaidi kwani hata wiki iliyopita tulikuwa na Mhe. Waziri wa Afya Ummy Mwalimu akizindua Mpango mkubwa wa kuboresha Afya ya Uzazi kwa Wajawazito na Watoto (IMPACT) unaotekelezwa na Aga Khan Development, Network kwa ufadhiri wa serikali ya Canada utakaogharimu shilingi Billioni 25 na kutekelezwa katika Halmashauri zote nane za wilaya 7 za mkoani Mwanza hii kwetu ni mafanikio makubwa,” alisema Dkt. Thomas.
Aidha, Dkt.Thomas ameongeza kuwa, serikali kwa kuwezesha kupata 96%-98% ya fedha ya madawa na vifaa Tiba kutokea 46% iliyokuwa ikitolewa huko nyuma imefanikisha sana kuboreha huduma ya afya, pia amekumbushia ahadi ya Mashine ya Mionzi (CT SCAN ) iliyoahidiwa Mhe. Waziri wa Afya na kumuomba Mhe. Naibu waziri kukumbushia kwani Chumba maalumu wa ajili ya mashine hiyo kimeandaliwa kama alivyoagiza.
Hata hivyo Mhe.Ndugulile ameziagiza hospitali zote nchini kuepuka kuwaandikia wagonjwa dawa ambazo hazipatikani maeneo ya huduma ili kuepukana na usumbufu.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.