Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa ameipongeza Kamati ya Usalama Barabarani Mkoa wa Mwanza kwa kununua gari na kulikabidhi jeshi la polisi ili litumike kufanya doria mkoani humo.
Waziri Mkuu Mhe. Majaliwa ametoa pongezi hizo leo jijini Mwanza wakati akizindua Wiki ya Nenda kwa Usalama Barabarani inayofanyika Kitaifa Katika Uwanja wa Furahisha Uliopo Wilaya ya Ilemela Mkoani Mwanza baada ya Mwenyekiti wa Kamati hiyo Frednand Chacha kumkabidhi gari hilo aina ya Land Cruiser ili amkabidhi Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini(IGP) Camillus Wambura.
“Nitoe shukrani zangu za dhati kwa Kamati ya Mkoa ambayo imetoa gari na kulipa jeshi la polisi kwa ajili ya kufuatilia mwenendo mzuri wa matumizi wa vyombo vya moto hapa mkoani Mwanza hongera sana Mhe Mwenyekiti wa Kamati Frednand Chacha kwa kushirikiana na kamati yako mmetumia fedha zenu na hatimaye gari limepatikana ambalo nimelipokea na kumkabidhi IGP.
“Natamani kila mwenye uwezo ambaye anaweza kuona umuhimu wa jeshi letu la polisi katika kusimamia usalama wetu barabarani akafanya kama ilivyofanya Kamati ya Usalama Babarani Mkoa wa Mwanza, Serikali itaendelea kuboresha miundombinu ya usafiri na usafirishaji lengo letu ni kurahisisha shughuli za usafirishaji,”amesema Mhe.Majaliwa.
Aidha amempongeza Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Adam Malima kwa kuunda kamati ambayo imeshirikiana na Kamati Kuu ya Kitaifa kuratibu maadhimisho hayo kwani yatawanufaisha wananchi wa mkoa huo na mikoa ya kanda ya ziwa kwa kupata elimu ya jinsi ya kutumia barabara ili kupunguza ajali.
Mhe. Majaliwa amewataka wananchi wote kufuata sheria kanuni na miongozo ya kutumia barabara ili kupunguza ajali kwani Takwimu za ajali barabarani zilizofikishwa kwenye vyombo vya usalama na kutolewa taarifa na jeshi la polisi kwa miaka mitatu iliyopita kuanzia Januari mwaka 2020 hadi Desemba, 2022 zilikuwa ni 5132 ziligharimu maisha ya watu 4060 na kusababisha majeruhi na walemavu 6427.
Aidha Mhe. Majaliwa ametoa jumla ya maagizo 13 kwa Baraza la Taifa la Usalama Barabarani ili kupunguza au kumaliza changamoto ya ajali za barabarani ikiwemo kuharakisha mchakato wa mapendekezo ya marekebisho ya sheria na kanuni za usalama barabarani ili kuwa na sheria bora isiyoacha mwanya kwa watumiaji wote wa barabara wanaotembeza vyombo bila kuzingatia sheria, kufuatilia kuanzishwa kwa mfumo wa kuweka alama kwenye barabara na leseni za udereva ili kuwabaini madereva wanaokiuka sheria na iwe rahisi kuwachukulia hatua.
“Pia Baraza litekeleze kwa ukamilifu maagizo ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan aliyoyatoa kwenye maadhimisho ya wiki ya nenda kwa usalama barabarani mwaka jana 2022 yaliyofanyika jijini Arusha kuhusu kuimarisha ukaguzi wa magari kwa kushirikisha sekta binafsi badala ya utaratibu wa sasa unaoshirikisha jeshi la polisi peke yake kukagua magari maana magari ni mengi,”amesema Mhe. Majaliwa na kuongeza.
“Jeshi la polisi Tanzania liharakishe ufungaji wa mifumo ya kielektroniki itakayokuwa inabaini makosa mbalimbali ambayo inasaidia kulinda mwenendo wa madereva wasiokuwa na maadili na pia itarahisisha ufanyaji kazi maana itatoa taarifa ni dereva yupi anayeendesha vyombo vya moto akiwa amelewa ,”amesisitiza Mhe. Majaliwa.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhe. Adam Malima amelishukuru Baraza la Taifa la Usalama Barabarani kwa kuuchagua mkoa huo kuwa mwenyeji wa maadhimisho ya wiki ya nenda kwa usalama barabarani na kubainisha kwamba watakuwa kinara wa kuheshimu sheria, kanuni na taratibu za Barabarani ambapo pia alimuomba Waziri Mkuu Mhe. Majaliwa kupeleka maadhimisho hayo mwakani mkoani humo.
Maadhimisho ya wiki ya nenda kwa Usalama Barabarani mwaka huu 2023, yanaongozwa na Kauli Mbiu Isemayo 'Tanzania bila ajali inawezekana -Timiza wajibu wako.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.