Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe Mhandisi Robert Gabriel leo tarehe 08 Juni, 2022 amekagua Mradi wa Maji Magulukenda uliotekelezwa na Wakala ya Usambazaji Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) kwa Tshs Milioni 150 katika Halmashauri ya Buchosa.
Akizungumza na viongozi baada ya kukagua Mradi huo uliowaondolea adha ya kupata maji mbali wananchi 5151 wa kijiji cha Magulukenda, Mkuu wa Mkoa ametoa wito kwa RUWASA na Halmashauri kutoa elimu kwa jumuiya ya watumia Maji pamoja na jamii inayozunguka Mradi huo ili waumiliki na kuutunza kizalendo uweze kuwasaidia kwa muda mrefu na kupunguza upotevu wa Maji.
"Serikali inaleta fedha nyingi sana tunaunda Jumuiya za watumia maji ili watunze Miundombonu hii hivyo tujiandae kwenye mazingira hayo na tuwe na taarifa ya mapato na matumizi kwa kufuata taratibu za kifedha maana vifaa vinaharibika wakati mwingine na kuhitaji matengenezo, tuweke akiba." amesisitiza.
Awali akiwasili kwenye Halmashauri hiyo, Mhe Mkuu wa Mkoa alikagua Kituo cha Mafuta cha Bulunda-Bukokwa kilichojengwa kwa Tshs. Milioni 220 na kusaidia wananchi kupata huduma hiyo jirani tofauti na awali ambapo walipata umbali wa KM 30 na amewataka viongozi wa Halmashauri hiyo kuhakikisha mwekezaji huyo ana nyaraka ikiwa ni pamoja na hati ya kiwanja.
Wananchi wa Sukuma-Bukokwa wanaojengewa barabara ya KM 12.5 na Wakala wa Barabara Vijijini na Mijini (TARURA) yenye thamani ya zaidi ya Milioni 200 ambayo imefikia asilimia 50 ya ujenzi wake walifikiwa na ziara hiyo na Mhe Mkuu wa Mkoa amemtaka Mkandarasi kuongeza nguvukazi kwenye ujenzi huo ili kukabiliana na changamoto ya mwenendo wa taratibu wa ujenzi.
Kabla ya Mkuu wa Mkoa kuwapa hamasa ya kufanya kazi kwa bidii Vijana wa kikundi cha 'Vijana na Maendeleo Nyehunge' kilichokopeshwa Tshs Milioni 6 na Halmashauri kwa shughuli za kufyatua Matofali, alikagua Maabara za Masomo ya Sayansi kwenye Shule ya Sekondari ya Nyehunge.
Pamoja na kukagua Mradi wa kampeni ya Lishe, Ziro Malaria na kampeni ya VVU/UKIMWI, Jengo la huduma ya dharula kwenye Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Buchosa linalotekelezwa kwa Tshs Milioni 300 limehitimisha ziara ya Mhe Mkuu wa Mkoa ambapo Dkt Rajab Amour Mganga Mfawidhi wa hospitali hiyo amebainisha kuwa litakapokamilika litasaidia kupunguza vifo kwa asilimia 40 kutokana na mfumo utaofungwa.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.