Mkuu wa Mkoa Mwanza, asitisha mkutano wa wadau wa elimu.
MKUU wa Mkoa wa Mwanza John Mongela amesitisha Mkutano wa wadau wa elimu uliokuwa ufanyike leo(jana) mkoani hapa baada ya baadhi ya Wakurugenzi na Maafisa elimu wa wilaya na manispaa kushindwa kuhudhuria kikao hicho na kuwatuma wawakilishi wao, jambo ambalo limemkera mkuu huyo wa Mkoa.
Akiwaomba radhi wadau wengine wa elimu waliohudhuria kikao hicho kwa usumbufu waliopata baada ya yeye kuahirisha kikao hicho , Mongela alisema hatua iliyoonyeshwa na Maafisa hao kutohudhuria kikao hicho muhimu ambacho kilikuwa kinajadili mambo ya elimu mkoani humo ni dharau kubwa iliyonyeshwa na watumishi hao kwake.
"Hivi kama mtu umealikwa kikao cha Mkuu wa mkoa ukadharau, hivi utahudhuria kikao gani kingine, Katibu Tawala (RAS) huu ni mzaha , haiwezekani tuitishe kikao zaidi ya miezi miwili halafu watu hawahudhurii", alifafanua.
Alisema kukosekana kwa Wakurugenzi na Mafisa elimu kwenye kikao hicho wakati hoja ambayo ilitakiwa kujadiliwa ni ya elimu inaonyesha ni jinsi gani mkoa unajiteng’enezea mazingira ya kufanya vibaya katika sekta ya elimu.
Alisema kwa tabia iliyoonyesha na watendaji hao na idadi ya wajumbe waliohudhuria kikao hicho, ambapo baadhi yao ni watu ambao hawalipwi mishahara na serikali, usingeleta tija.
“ Unajua nimekwazika sana, niwatake radhi sana, naahirisha kikao hiki hadi hapo kitakapoandaliwa tena kwa gharama za Wakurugenzi ambao hawakuhudhuria kwenye kikao hiki, wataalikwa wajumbe na kwa wanaotoka mbali watawasafirisha kuja kikao kitakachofuata”, alisema, na kuongeza,
“Haiwezekana tukaenenda katika utendaji wa aina hii, jambo lenyewe elimu, haiwezekani Mkurugenzi wa halmashauri, Afisa elimu msingi na sekondari wasiwepo kwenye kikao hiki, huu ni ukosefu wa nidhamu”,
Alitumia fursa hiyo kuwakumbusha watendaji wa serikali mkoani kwake kuacha kufanya kazi kwa mazoea ambapo alisisitiza kuwa wakati huu wa Serikali ya awamu ya tano lazima waepuke mizaha ya aina hiyo.
Tena watu ambao hawakuhudhuria ni watu ambao wanalipwa mishahara na serikali na ambao wamehudhuria ambao ni wengi ni wale ambao hawalipwi mishahara na serikali, na ndio maana tunashindwa kumaliza ujenzi wa madarasa na tatizo la madawati na shule zetu nyingi zinafeli, hili jambo sitaki tena lijirudie kwenye mkutano ujao’, alisema.
Miongoni mwa viongozi ambao hawakuhudhuria kwenye mkutano huo muhimu wa kujadili mambo ya elimu ni Wakurugenzi watendaji na Maofisa elimu wa halmashauri za Misungwi, Ukerewe na Manispaa ya Ilemela ambao waliwakilishwa na maafisa wengine wa halmashauri hizo hoja ambayo ilionekana ni dhaifu kulingana na umuhimu wa kikao kilichokuwa kinajadili mambo ya elimu kimkoa.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.