HADI KUFIKA DISEMBA TUNATARAJIA KUTOA CHANZO KWA WATOTO WA KIKE ZAIDI YA MILIONI 4 : WAZIRI UMMY
Waziri wa Afya Mhe: Ummy Mwalimu (MB) leo Aprili 22, 2024 amezindua rasmi Maadhimisho ya wiki ya chanjo Kitaifa ya Saratani ya mlango wa kizazi kwa watoto wa kike kuanzia miaka 9-14 na kusema mpango wa Serikali hadi kufika Disemba mwaka huu wanatarajia kufikia idadi ya watoto zaidi ya milioni 4.
Akizungumza kwenye uzinduzi huo Mkoani Mwanza katika viwanja vya Furahisha, Mhe. Ummy amesema Maadhimisho yanakwenda kwa kutoa dozi mara moja tu tofauti na hapo awali walitoa dozi mara mbili na hii ni kutokana na utafiti wa kitaalamu uliofanywa hapa nchini na baadaye kuridhiwa na Shirika la Afya Duniani WHO.
"Tanzania ni ya nne Duniani kwa tatizo hili la Saratani ya shingo ya kizazi, takwimu zinaonesha katika wagonjwa 100 wa Saratani, 25 wana tatizo la Saratani ya shingo ya kizazi tuna wajibu wa kutokomeza hali hii na tuepuke upotoshaji wowote wa chanjo hii", Waziri Ummy.
Amesema Serikali ina nia njema ya kuhakikisha Taifa linakuwa salama na lenye watu wenye afya bora,ndiyo maana chanjo hii ni bure na haihusiani na uzazi wa mpango kama baadhi wanavyodhania.
"Nawasihi sana nyie wanangu mliopo hapa epukeni ngono kabla ya wakati wake,wengi wenu mnapata tatizo hili kutokana na kuyakimbilia haya mambo mapema na matokeo yake mnaingia katika gharama kubwa ya matibabu ya saratani,"amesisitiza Waziri wa Afya.
Aidha amewataka wazazi kuiunga mkono Serikali katika wiki hii ya kampeni kwa kuhakikisha watoto hao wanapata chanjo itakayo muweka salama katika maisha yake.
Awali kabla ya kumkaribisha mgeni rasmi Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana Mhe:Amina Makilagi aliyemuwakilisha Mkuu wa Mkoa ameishukuru Serikali kwa kuleta miradi ya Afya yenye gharama ya zaidi ya shs bilioni 48 na kumuhakikishia Waziri Ummy miradi hiyo itasimamiwa kikamilifu na kukamilika kwa wakati ili iwe na tija kwa wananchi.
"Mhe: Waziri tuna vituo 400 vinavyotoa chanjo Mkoani hapa na Machi 2024 tumetoa chanjo kwa watoto 37213,na wiki hii ya kampeni tutahakikisha tutazingatia maelekezo yote ya Serikali ili kutimiza malengo ya kuwa na Taifa lenye watu salama," Mhe:Makilagi
Mdhibti ubora wa shule kanda ya ziwa Bi.Lucy Nyanda amesema wamejipanga vizuri kuhakikisha malengo ya kufaniikisha kampeni ya chanjo ya Saratani ya mlango wa kizazi inafanyika kwa ubora na kwa walengwa wote.
"Wazazi wenzangu naomba tuelewane katika hili jambo tujiepushe na maneno ya upotoshaji kuhusiana na kampeni za chanjo,tuendelee kuelimika na kuzingatia maelekezo yote sahihi yanayotolewa na Serikali",Mdhibti ubora.
Kila mwisho wa jumla la Aprili Tanzania inaungana na Mataifa Duniani katika Maadhimisho ya chanjo ya Saratani ya mlango wa kizazi
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.