Sunday 22nd, December 2024
@Tanzania na Zanzibar
HISTORIA YA MUUNGANO WA TANGANYIKA NA ZANZIBAR
Historia, sababu na Hati za Muungano Jamhuri ya Muungano wa Tanzania iliundwa mnamo tarehe 26 Aprili 1964 kwa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar inayojumuisha Visiwa vya Pemba na Unguja 27/05/2009 HISTORIA YA MUUNGANO WA TANGANYIKA NA ZANZIBAR Jamhuri ya Muungano wa Tanzania iliundwa mnamo tarehe 26 Aprili, 1964 kwa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar (inayojumuisha Visiwa vya Pemba na Unguja). Tanganyika ilikuwa ni mwendelezo wa koloni la Ujerumani, utawala wa Waingereza kwa Mamlaka ya Umoja wa Mataifa, Himaya ya Umoja wa Mataifa chini ya utawala wa Uingereza na mwisho Taifa huru kuanzia mwaka 1961 ndani ya nchi za Jumuiya ya Madola. Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar ziliingia mkataba wa Muungano mnamo mwaka 1964 na kuanzishwa Dola ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mkataba huu wa Muungano ulitiwa saini na aliyekuwa Rais wa Tanganyika, Hayati Mwalimu Julius Nyerere na aliyekuwa Rais wa Zanzibar, Hayati Sheikh Abeid Amani Karume tarehe 22 Aprili 1964 huko Zanzibar. Mkataba huo ulithibitishwa na Bunge la Tanganyika na Baraza la Mapinduzi hapo tarehe 26 Aprili, 1964 na mnamo tarehe 27 Aprili, 1964, viongozi wa nchi zote mbili walikutana katika ukumbi wa Karimjee Jijini Dar es Salaam na kubadilishana Hati za Muungano.
Sheria za Muungano zilitoa tamko la Jamhuri ya Muungano katika Ibara ya 4 kwamba: “Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar zitalazimika, baada ya kuungana na siku zote baada ya kuungana, kuunganishwa kuwa Dola ya Jamhuri kwa jina la Jamhuri ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar’ (Ibara ya 4 Sheria za Muungano) 2 Jina hili la “Jamhuri ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar” lilibadilishwa baadae mnamo tarehe 28 Oktoba, 1964 na kuwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kupitia Sheria ya Jamhuri ya Muungano, Sheria namba 61 ya mwaka 1964.
Watanganyika kama ilivyokuwa kwa wananchi wa nchi nyingine za kiafrika, hawakukubaliana hata kidogo na utawala wa kikoloni. Tangu mwanzo waliwapinga na kupigana na wavamizi wa kikoloni, upinzani mkubwa ukionyeshwa na Wasambaa wakiongozwa na Kimweri dhidi ya Wajerumani, Wahehe wakiongozwa na Mkwawa kupigana vichungu na virefu dhidi ya Wajerumani na wakati wa vita vya Maji Maji chini ya uongozi wa Kinjekitile, Mputa na Kibasila. Kukosekana kwa umoja kati ya wapigania uhuru hawa wa mwanzo na uimara wa majeshi ya wakoloni na silaha bora za moto kulidhoofisha mapambano haya ya uhuru na kusababisha hasara kubwa na kupoteza maisha ya watu.
Kama ilivyokuwa kwenye makoloni mengi ya Kiafrika, hisia za Utaifa ziliendelea kuimarika katika Tanganyika baada ya mwaka 1945. Alama za utaifa zilishaanza kuonekana punde baada ya vita kuu ya kwanza ya dunia kwa kuanzishwa kwa vyama mbalimbali vya Waafrika kwa upande wa Tanganyika na Zanzibar. Kwa upande wa Tanganyika, African Association ilianzishwa mwaka 1929 kama kikundi cha mijadala baina ya wasomi na ilipofika mwaka 1948 chama hiki kikawa Tanganyika African Association (TAA).
Baada ya vita ya Pili ya Dunia, wanachama wa Tanganyika African Association 3 (TAA) waliendeleza wimbi la utaifa. Mwaka 1953 chini ya uongozi wa Mwalimu Nyerere, TAA ilitambuliwa kama chama cha siasa na kuelekea moja kwa moja kuanzishwa kwa TANU mwaka 1954 iliyotumika kama chombo cha kisiasa cha watu katika kutoa vilio vyao vya kudai uhuru. Kuanzishwa kwa TANU mwaka 1954, ulikuwa ndio mwanzo wa mbio za kupigania uhuru. Baada ya miaka saba ya mapambano ya kisiasa, Tanganyika ilikuwa huru chini ya chama cha TANU,kilichoimarishwa na vyama vya wafanyakazi na vya ushirika. Kwa upande wa Zanzibar, chimbuko la Jumuiya ya Waafrika ilikuwa ni vilabu vya mpira wa miguu vilivyoanzishwa mwanzoni mwa miaka ya 1930. Ilipofika mwaka 1934, Jumuiya ya Waafrika ilianzishwa rasmi na kupewa jina la African Association (AA).
Baada ya vita ya pili ya dunia kama ilivyokuwa katika sehemu nyingine za dunia, kulikumbwa na uhaba mkubwa wa chakula, ubaguzi na mgawanyiko baina ya jamii. Kutokana na matatizo hayo ya ubaguzi, kulianzishwa Jumuiya ya Washirazi (Shirazi Association) katika Visiwa vya Unguja na Pemba lengo likiwa ni kudai kupatiwa haki mbalimbali za kijamii na kulinda utambulisho wao. Kuundwa kwa chama cha ZNP (Zanzibar Nationalist Party) mwaka 1957, kulifanya viongozi wa Jumuiya ya Waafrika (African Association) na wale wa Shirazi Association waone umuhimu wa kushirikiana. Waligundua kuwa Serikali ya kikoloni na chama cha ZNP walishirikiana kuendeleza dhuluma dhidi ya Waafrika. Viongozi hao waliona ulazima wa kuungana kuwa kitu kimoja kupigania uhuru. Hivyo, katika kutekeleza azma hiyo, Viongozi wa Jumuiya hizo walikutana na kukubaliana kuunganisha Shirazi Association na African Association mwaka 1957 4 na kuunda chama kilichoitwa Afro- Shirazi Union ambacho baadae kiliitwa Afro-Shirazi Party chini ya uongozi wa Sheikh Abeid Amani Karume. Mwalimu Nyerere alishiriki katika mkutano huu.
Ilikuwa tarehe 05 Desemba, 1957 hapo mtaa wa Mwembekisonge Unguja. Kati ya mwaka 1957 mara tu baada ya uchaguzi mkuu wa kwanza na mwishoni mwa mwaka 1963, kabla ya mapinduzi ya mwaka 1964, Zanzibar ilitawaliwa na vuguvugu na mivutano mikali ya kisiasa. Mapambano haya ya kisiasa yalikuwa kati ya Chama cha Afro-Shirazi kilichoungwa mkono na Waafrika na kile cha Zanzibar Nationalist Party kilichoungwa mkono na Wakoloni, Sultani pamoja na jamii ya Waarabu.
Chama cha ZNP baada ya kushindwa uchaguzi, kilianzisha kampeni za kushawishi wenye mashamba na mabepari wengine wenye kumiliki njia kuu za uchumi, kuwafukuza kazi au kutowaajiri wafuasi wa ASP. Halikadhalika, Chama cha ZNP kiliwatafutia kazi na kuwabakisha mashambani Waafrika wote waliokubali kukiunga mkono. Wakati wa mvutano huo wa kisiasa kati ya ASP na ZNP ikipamba moto, kulijitokeza tofauti miongoni mwa viongozi wa ASP.
Tofauti hizo zilichangiwa na uroho wa madaraka, ubinafsi na kutokuwa na msimamo imara miongoni mwa baadhi ya viongozi wa chama hicho. Halikadhalika Serikali ya Sultani nayo ilichochea migogoro hiyo ili ijinufaishe kisiasa. Migogoro hiyo ilipelekea kujitoa kwa baadhi ya Viongozi wa ASP ambao walifanya mkutano na baadhi ya wanasiasa mashuhuri wa ASP huko Pemba Novemba, 1959 na kukubaliana kuanzisha Chama kipya cha siasa cha Zanzibar and Pemba People’s Party (ZPPP) na Sheikh Muhammed Shamte kuwa Mwenyekiti. Wakati vyama vya ASP, ZNP na ZPPP vikiwa katika malumbano makali ya kisiasa, Serikali ya Kikoloni ilifanya 5 matayarisho ya uchaguzi wa pili.
Uchaguzi ulifanyika tarehe 16 Januari, 1961 na siku moja kabla ya uchaguzi huo Serikali ilitangaza kuwa chama kitakachoshinda kitaunda Serikali na Wizara zote zitakuwa chini yake. Katika uchaguzi huo ASP ilishinda kwa kupata viti 10, ZNP kilipata viti 9 na chama cha ZPPP kilipata viti 3. Kutokana na kuenea kwa chuki za kisiasa miongoni mwa Wazanzibari, Vyama vikuu vya kisiasa vilifikia muafaka wa kumaliza hali hiyo. Hatahivyo, ASP haikufikisha zaidi ya nusu ya kura na hivyo haikuweza kuunda Serikali.
Hivyo njia pekee iliyobakia ilikuwa ni kuishauri ZPPP ichanganye viti vyake na chama kimoja kati ya ASP na ZNP. ZPPP na ZNP viliungana. Hatahivyo, iliamuliwa kuwa iundwe Serikali ya muda na kusubiri uchaguzi mwingine uliopangwa kufanyika mwezi Juni, 1961. Waingereza walitoa uhuru kwa Serikali ya Mseto ya ZNP/ ZPPP ya Waziri Mkuu Muhammed Shamte. Chini ya ushauri wa Waingereza, Shamte aliwatenga ndani ya Serikali yake baadhi ya viongozi wa ZNP wenye msimamo wa Kikomunisti wakiongozwa na Abdulrahaman Babu, na hivyo kutokea kutofautiana kwa baadhi ya viongozi wa ZNP na Serikali ya ZNP/ZPPP. Baada ya kutengwa na Serikali hiyo walijitoa ZNP na kuanzisha Chama cha Umma. Chama hicho kilivunjwa mara tu baada ya Mapinduzi ya mwaka 1964 na hapo viongozi na wafuasi wake walijiunga na Serikali ya ASP chini ya uongozi wa Abeid Karume.
Zanzibar ilikuwa na wakati mgumu katika kupigania uhuru. Waingereza walijikita zaidi kwa madhumuni ya kibiashara na kwa nia ya kukomesha biashara ya utumwa. Hii ilikuwa ni kwasababu, walitaka nguvukazi rahisi ambayo ilikuwa inapotea kwa kufanywa 6 watumwa kwa uzalishaji wa malighafi kwa ajili ya viwanda vyao Ulaya, halikadhalika kutokana na Mapinduzi ya Viwanda Ulaya yalisababisha Waingereza kuja kutafuta soko kwa ajili ya bidhaa zao. Waingereza walifikia makubaliano na Sultani mwaka 1822 ili kukomesha biashara ya utumwa, lakini ilichukua zaidi ya miaka 50 hadi utumwa kutokomezwa. Makubaliano ya Waingereza na Wajerumani ya mwaka 1890 yalifanya Zanzibar kuwa koloni la Waingereza ambao walimshirikisha Sultani katika utawala wao. Waingereza waliainzisha ubaguzi wa rangi Zanzibar kwa Wazungu na Waarabu kupendelewa kuwa tabaka la juu na Waafrika la chini.
Waingereza walifanya Zanzibar kuwa ni koloni la Waarabu na ilipofika Desemba 1963, Sultani alipewa mamlaka kamili ya kutawala Zanzibar. Tarehe 12 Januari 1964, aliyekuwa Sultani wa Zanzibar, Jamshid bin Abdulla, aling’olewa madarakani katika Mapinduzi yaliyokuwa yameandaliwa kwa usiri, ustadi na ujasiri mkubwa wa Wanamapinduzi wa Afro-Shirazi Party (ASP) na Jamhuri ikatangazwa. Muundo wa Muungano wa Tanzania kama ulivyoelezwa katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, una vyombo viwili vyenye mamlaka ya utendaji ambavyo ni Serikali ya Jamhuri ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Vyombo viwili vyenye mamlaka ya kutekeleza utoaji haki ambavyo ni Mahakama ya Jamhuri ya Muungano na Mahakama ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar; na vyombo viwili vyenye mamlaka ya kutunga sheria na kusimamia utekelezaji wa shughuli za umma ambavyo ni Bunge na Baraza la Wawakilishi. Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania 7 inashughulikia mambo yote ya Muungano kama yalivyoainishwa katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 na yasiyo ya Muungano kwa upande wa Tanzania Bara na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inayoshughulikia mambo yote yasiyo ya Muungano kwa upande wa Tanzania Zanzibar.
Muungano wa Tanzania ni tukio la nadharia iliyotafsiriwa katika vitendo, kwani kuunganisha Tanganyika na Zanzibar ilikuwa ni hatua ya watu walio wakweli. Ni ushahidi unaojitosheleza kuwa wananchi wa Tanganyika na wa Zanzibar wakiongozwa na viongozi wao wa mapambano ya kudai uhuru, walitoa kauli zilizokuwa zikimaanisha walichofikiri na kuazimia na wala siyo kwa sababu ya kusombwa na jazba za kisiasa. SABABU ZA KUWEPO KWA MUUNGANO Muungano wa Tanganyika na Zanzibar umekuwepo kutokana na sababu zifuatazo:-
1. Kuwepo kwa mahusiano ya karibu kihistoria baina ya Tanganyika na Zanzibar katika nyanja mbalimbali kama vile udugu wa damu, biashara, utamaduni, lugha na mahusiano ya karibu kisiasa hususan baina ya TANU na ASP. 2. Moyo wa kuwa na Muungano wa Afrika hususan kwa kuanzia na Shirikisho la Afrika Mashariki. Hata kabla ya uhuru wa Tanganyika, Mwalimu Nyerere pamoja na viongozi wengine 8 waliokuwa wakipigania utaifa katika ukanda wa Afrika Mashariki walikuwa na matarajio ya kuwa na Muungano wa Afrika. Mwalimu Nyerere binafsi alipendelea uwepo Muungano wa Afrika kwa kuanzia na Mashirikisho ya kikanda.
Baada ya kushauriana na viongozi mbalimbali wa iliyokuwa Jumuiya ya Wapigania Uhuru wa Afrika Mashariki na Kati (Pan- African Freedom Movement for East and Central Africa - PAFMECA) Mwalimu Nyerere alitoa tamko wakati wa mkutano wa nchi huru za Afrika uliofanyika Addis Ababa mwaka 1960 kwamba; “Wengi wetu tunakubaliana bila kikwazo kwamba Shirikisho la Afrika Mashariki litakuwa ni jambo zuri. Tumesema na ni kweli kwamba mipaka inayotenganisha nchi zetu imewekwa na mabeberu na sio sisi wenyewe na kwamba tusikubali itumike dhidi ya umoja wetu…lazima tuzisumbue ofisi za wakoloni kwa nia si ya kudai uhuru wa Tanganyika, kisha Kenya, na Uganda halafu Zanzibar lakini kwa nia ya kutaka uhuru wa Afrika Mashariki kama Muungano mmoja wa Kisiasa”.(imeripotiwa kwenye gazeti la Tanganyika Standard, Novemba 1964) Mapinduzi ya Zanzibar mnamo mwezi Januari, 1964 yalifanyika wakati Mwalimu Nyerere akiwa ameshachoshwa na kukatishwa tamaa na mazungumzo ya Shirikisho la Afrika Mashariki. Mapinduzi haya yaliiweka madarakani Serikali ya chama cha ASP kilichokuwa na mahusiano ya karibu na TANU kwa upande wa Tanganyika.
Kwa uhakika zaidi, upo mchanganyiko wa sababu mbalimbali za Muungano huu kama vile historia za nchi hizi mbili, ukaribu 9 wa nchi hizi mbili, muingiliano wa kijamii, ushirikiano wa kibiashara, ushirikiano madhubuti na wa muda mrefu wa kisiasa baina ya TANU na ASP, ushirikiano na urafiki wa muda mrefu kati ya watu, viongozi, na wakati wa harakati za utaifa uliopelekea uhuru wa nchi hizo mbili, sababu za kiusalama n.k. HATI YA MAKUBALIANO YA MUUNGANO Msingi wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 na Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 ni Hati za Muungano za mwaka 1964. Hati za Muungano zilitiwa saini na waasisi wa Muungano tarehe 22 Aprili, 1964, na hapo Tanganyika na Zanzibar kuwa dola moja, ya Jamhuri ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar. Mapatano ya Muungano yaliunganisha mataifa mawili yaani Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya watu wa Zanzibar na kuweka Taifa moja la Jamhuri ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar kwa misingi ya Katiba na misingi inayotambulika Kimataifa. Jina la Jamhuri ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar lilibadilishwa baadae na kuwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Baada ya Muungano, Mwalimu J. K. Nyerere alikuwa Rais wa kwanza na Sheikh Abeid Amani Karume, alikuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Tarehe 26 Aprili, 1964 Bunge la Tanganyika lilipitisha Sheria za Muungano. Halikadhalika Sheria hizi zilithibitishwa na Baraza la Mapinduzi Zanzibar. Sheria hizi za Muungano zilithibitisha Hati za Muungano, zilitaja Rais na Makamu wa Rais, zilitaja Muundo wa Muungano na Katiba ya Muungano. Mnamo tarehe 27 Aprili 1964, 10 waasisi wa Muungano walibadilishana Hati za Muungano na wajumbe saba (7) wa Baraza la Mapinduzi waliapishwa kuwa Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ambao ni: Sheikh Abeid Amani Karume, Bw. Kassim Abdala Hanga, Bw. Abdulrahaman Mohamed Babu, Sheikh Hassan Nassor Moyo, Sheikh Aboud Jumbe, Sheikh Hasnu Makame na Sheikh Idris Abdul Wakil. Wote hawa walifanya Mawaziri wa Serikali ya Muungano. Kati ya Viongozi hawa wawili wako hai hadi sasa. Nao ni Aboud Jumbe na Hassan Nassor Moyo. Kabla ya siku ya Muungano, kulikuwa na Katiba mbili; Katiba ya Tanganyika ya mwaka 1962 na upande wa Zanzibar kulikuwa na Amri za Katiba (Constitution decrees).
Katiba ya Tanganyika baada ya kufanyiwa marekebisho iliendelea kutumika kama Katiba ya Muungano wakati ule wa mpito, kuanzia tulipoungana hadi ilipopitishwa Katiba ya Muungano kwa mujibu wa Makubaliano ya Muungano na Sheria za Muungano. Aidha, marekebisho hayo yalimtaja Rais wa Zanzibar kuwa ni Makamu wa kwanza wa Rais, akiwa ni msaidizi wa Rais kwa masuala yote ya kiutawala kwa upande wa Zanzibar, na Waziri Mkuu kuwa ni Makamu wa Pili wa Rais ambaye atamsaidia Rais kwa masuala yahusuyo upande wa Tanganyika na kiongozi wa shughuli za Serikali Bungeni. Katiba ya muda ya mwaka 1965 ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania iliainisha mambo kumi na moja (11) ambayo yalikubalika kuwa ni ya Muungano chini ya usimamizi wa Serikali ya Muungano. Mambo hayo ni; 11 •
Katiba na Serikali ya Muungano • Mambo ya Nchi za Nje • Ulinzi • Polisi • Mamlaka juu ya mambo yanohusika na hali ya hatari • Uraia • Uhamiaji • Mikopo na Biashara ya Nchi za Nje • Utumishi katka Serikali ya Jamhuri ya Muungano • Kodi ya Mapato inayolipwa na watu binafsi na mashirika, ushuru wa forodha na ushuru wa bidhaa zinazotengenezwa nchini Tanzania unaosimamiwa na Idara ya Forodha. • Bandari mambo yanayohusika na usafiri wa anga, posta na simu. Katiba ya muda ya mwaka 1965 ilianiainisha utawala wa Serikali ya mfumo wa chama kimoja, TANU kwa Bara na ASP kwa Zanzibar. Katiba hii, ilizingatia misingi ya Makubaliano ya Muungano ya mwaka 1964 na Sheria za Muungano wa Tanganyika na Zanzibar. Katiba ya muda ya mwaka 1965 iliainisha Serikali mbili, Uwakilishi wa Zanzibar katika Bunge la Muungano na uongozi wa Serikali ya Zanzibar.
Serikali ya Muungano ikiwa na mamlaka juu ya mambo yote ya Muungano na mambo yote yasiyo ya Muungano kwa upande wa Tanganyika. Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ikiwa na mamlaka juu ya mambo yote yasiyo ya Muungano yahusuyo Zanzibar. 12 KUONGEZEKA KWA MAMBO YA MUUNGANO Mambo ya Muungano yaliongezeka kutoka kumi na moja (11) hadi ishirini na mbili (22) kutokana na mahitaji ya ndani ya wananchi yaliyolenga kuunganika kwa mambo mengi zaidi pamoja na mabadiliko yaliyokuwa yanaendelea kutokea ulimwenguni baada ya Muungano. Mwaka 1965, jambo la kumi na mbili linalohusu Mambo yote yanayohusika na sarafu na fedha kwa ajili ya malipo yoyote halali (pamoja na noti); mabenki (pamoja na mabenki ya kuweka akiba) na shughuli zote za mabenki; fedha za kigeni na usimamizi juu ya mambo yanayohusika na fedha za kigeni liliongezeka chini ya Katiba ya muda ya mwaka 1965.
Sababu kubwa ilikuwa ni kuwa na sarafu ya pamoja ya Tanzania baada ya Muungano, na kurahisisha usimamizi wa fedha za kigeni na mabenki katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Aidha, kufuatia kuundwa kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki mwaka 1967, mambo matatu ya Muungano yaliongezwa, ambayo ni; Leseni za viwanda na takwimu; elimu ya juu; na usafiri na usafirishaji wa anga. Mwaka 1968, mambo ya maliasili ya mafuta, pamoja na mafuta yasiyochujwa ya motokaa na ama ya petrol na aina nyinginezo za mafuta au bidhaa na gesi asilia yaliongezwa kwenye orodha ya mambo ya Muungano. 13 Aidha mambo ya Muungano yaliendelea kuongezeka hadi kufikia 21 kufuatia kuvunjika kwa iliyokuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki mwaka 1977. Mambo yote yaliyokuwa ya upande wa Tanganyika na Zanzibar yaliyokuwa yakisimamiwa na Jumuiya ya Afrika Mashariki, yalikabidhiwa kwa Serikali ya Muungano. Mwaka 1992 kufuatia mabadiliko ya mfumo wa siasa nchini suala la ishirini na mbili la uandikishaji wa vyama vya siasa na mambo mengine yanayohusiana navyo liliongezwa kwenye orodha ya mambo ya Muungano. 14
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.