Waziri Mkuu wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (MB) ametoa pole kwa wananchi wa Mkoa wa Mwanza kwa kuharibiwa mali zao, kusababishiwa hasara na kukosa huduma muhimu za kijamii.

Dkt. Nchemba ametoa pole hiyo wakati akikagua Kiwanda cha magodoro cha Banco pamoja na Ofisi ya Maboto microfinance katika Wilaya za Nyamagana na Ilemela ikiwa ni miongoni mwa mali za wananchi zilizoharibiwa katika vurugu zilizojitokeza Octoba, 29, 2025.

Dkt. Nchemba amesema kuwa analaani vitendo vya uvunjifu wa amani na vurugu zinazorudisha nyuma amani kwani kwa kipindi kirefu Tanzania imekua ikifahamika kama kisiwa cha utulivu.

Aidha amewataka wananchi kujutia matendo waliyoyafanya na ametoa wito kwa kila mmoja kuwa mlinzi wa mwenzie na kuhakikisha vijana wanakemewa kwa matendo hayo kwani yana madhara makubwa kwa taifa.

Sambamba na hayo Dkt. Nchemba amesema baada ya kufanyika tathmini ya kina juu ya uharibifu uliofanyika, serikali itatoa tamko rasmi kuhusu hatua zipi zitachukuliwa pia ameahidi kuwa, watahakikisha wanaimarisha maswala ya kiusalama katika nchi ili kuhakikisha uharibifu wa namna hio haujitokezi tena.

Akikagua uharibifu uliofanywa kwenye ofisi ya mtendaji wa kata ya Nyasaka wilayani Ilemela Dkt. Nchemba amewataka wananchi kutokubali kurubuniwa na watu wasioitakia mema nchi.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda amesema uharibifu wa ofisi ya mtendaji wa kata hio ya Nyasaka umepelekea wananchi zaidi ya elfu 41 kukosa huduma huku uongozi wa kata ukipata hasara ya Shilingi milioni 35.

Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.