Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Mpango ameiagiza Wizara ya Maji kuondoa kero ya Upatikanaji Maji kwa wananchi wa Wilaya ya Ukerewe kwa kusimamia kwa ukaribu mradi Mkubwa wa Maji Kaziranganda wenye thamani ya Bilioni 7 na miradi mingine 11 inayotekelezwa ili ikamilike kwa ufanisi.
Dkt. Mpango ametoa agizo hilo leo (Novemba 25, 2022) wilayani humo wakati akihutubia wananchi wa Wilaya hiyo kwenye viwanja vya Getrude Mongela wakati akihitimisha ziara yake ya kikazi ya Siku nne Mkoani Mwanza.
Aidha, amemuagiza Mhe. Silinde kukagua mwenendo wa Uendeshaji wa Halmashauri ya Ukerewe kwani umekua na malalamiko mengi ya ubadhirifu. "Fedha za Miradi zitumike ipasavyo, nataka wanaodokoa wachukuliwe hatua zinazostahili na wakiwashinda waleteni kwangu mutaona nitakachowafanya" Amesisitiza Dkt. Mpango.
Vilevile, ameiagiza wizara ya Ujenzi kuanza Ujenzi wa Barabara ya Nansio, Kibara, Bunda na daraja la Kisorya kwenye mwaka wa fedha ujao kwani ufanisi kwa ajili ya Ujenzi huo ulishafanyika na amemtaka Waziri wa Afya kuchunguza Ujenzi wa Hospitali ya Nansio iliyopelekewa Bilioni 3 na kudaiwa kuhujumiwa hatua kali zichukuliwe kwa wahusika.
Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhe. Meja Jenerali Suleiman Mzee (Mkuu wa Mkoa Mara) amemshukuru Mhe. Makamu wa Rais kwa ziara yake Mkoani Mwanza na amemuahidi kuyafanyia kazi maagizo yote aliyoyatoa kwa viongozi Mkoani humo.
Naibu waziri wa Maji, Mhe. Maryprisca Mahundi amesema wilaya ya Ukerewe inapata huduma a maji kwa asilimia 56 ya mahitaji ya wananchi wake na kwamba wizara hiyo itaendelea kutekeleza miradi ya maji kwa ufanisi mkubwa na hasa kurekebisha mfumo wa uendeshaji wa mradi mkubwa wa Maji wa Bilioni 7 na miradi yote 11 midogo inayoendelea kutekelezwa kwa zaidi ya Bilioni 16.
Akizungumzia suala la kuanzishwa kwa Mji mdogo wa Nansio, Naibu Waziri TAMISEMl, David Silinde amesema jukumu hilo hufanywa na Halmashauri Mama na kwamba Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe ina mapato duni ambayo hayawezi kuendesha mamlaka hiyo Mpya na kwamba kuna taratibu zinaendelea ili kupata ufumbuzi wa suala hilo.
Aidha, amewapongeza viongozi wa Halmashauri hiyo kwa kujenga Miundombinu ya madarasa hasa kwenye shule za kata zote ambapo suala hilo litasaidia kuwezesha wananfunzi kujiunga kidato cha kwanza wote wakltakaofaulu kutokana na uwepo wa Miundombinu ya kutosha.
Mwenyekiti wa CCM Mkoa, Mhe. Reuben Sixbeth amesema kuwa Ukerewe imetekelwza Ilani kwa zaidi ya asilimia 60 kwa kutekeleza Miradi mbalimbali na akatumia wasaa huo kuitaka Kamati ya Siasa Wilaya hiyo kufuatilia kwa kina Miradi wa Maji yenye thamani ya Bilioni 7 ambayo inasuasua na Ujenzi wa Hospitali ya wilaya ambayo pamoja na uwepo wa fedha bado haiendi vema.
Mbunge wa Jimbo la Ukerewe Mhe. Joseph Mkundi ameishukuru Serikali kwa kuwaletea wananchi wa Jimbo hilo fedha za kutekeleza miradi Mbalimbali ya Maji, Elimu, Kilimo, Nishato ya Umeme, Barabara na Afya na kwa upekee ameshukuru kupata Pampu mbili mpya kwenye mradi mkubwa wa maji ambao sasa utaweza kuzalisha maji ya kutoshaleleza wananchi.
"Juzi mmetusaidia tani 300 kwa ajili kwa ajili ya kuwasaidia wananchi, tunashukuru sana kwa jambo hili ila tunaomba jambo moja nyeti la kujengewa ujenzi wa Barabara ya Kisorya kuja Nansio kwani ni sehemu muhimu sana kwa wananchi wa Ukerewe." Mhe. Mkundi.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.