Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki Bi. Edith Mwaje (Uganda) amesema jumuiya hiyo itahakikisha mradi wa mawasiliano na uchukuzi katika ziwa victoria unakamilika kwa wakati ili kuwa na kituo imara cha utafutaji, ufuatiliaji na uokozi kwa maslahi ya wavuvi na watumiaji ziwa victoria katika nchi wanachama.
Ametoa kauli hiyo mapema leo tarehe 11 agosti, 2025 katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza mara baada ya kujitambulisha, kufuatia ziara yake pamoja na ujumbe alioambatana nao ikiwa ni mahususi katika Mradi wa kimataifa wa mawasiliano na uchukuzi katika ziwa victoria pamoja na mingine ya kimkakati.
Bi. Mwaje amesema Wavuvi na wasafirishaji ndani ya ukanda wa ziwa victoria wana haki ya kulindwa wakati wote jambo ambalo jumuiya imelipa kulipaumbele kwa kujenga kituo maalumu pamoja na kuweka boti za kisasa za uokozi na ufuatiliaji pamoja na matibabu ndani ya ziwa hilo.
Aidha, ametumia jukwaa hilo kuwamwagia sifa viongozi wa Mkoa huo wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa kwa kuufanya mji nadhifu na wenye miradi kabambe ya kimkakati kama daraja la JP Magufuli ambalo limesaidia kuwaondolea adha ya usafiri wananchi wa ukanda huo.
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa, Katibu Tawala wa Mkoa huo Ndugu Balandya Elikana amesema serikali ya Tanzania ni mnufauka mkubwa wa mradi huo kwani utasaidia kuwalinda wavuvi na kuwakamata majangili ndani ya ziwa victoria kwa kulinda vizimba vya ufugaji samaki dhidi ya majangili na maharamia.
Ameongeza kuwa serikali imejiandaa na matunda chanya ya mradi huo kwani ndani ya ziwa victoria kuna miradi lukuki ya uvuvi kama boti za kisasa zilizotolewa kwa wavuvi kwa mkopo ambazo zinazingatia viwango vya kimataifa vya uhifadhi wa mazingira mbavyo vitapata uhakika wa msaada wakati wa majanga.
Aidha, amebainisha kuwa huduma za usafirishaji ndani ya ziwa hilo baina ya mikoa ya kanda ya ziwa pamoja na nchi rafiki unaendelea kuimarishwa kwani Mamlaka ya Bandari inajenga gati la kisasa lenye uwezo wa kupokea meli kubwa katika bandari za Mwanza Kaskazini na Kemondo na Bukoba ambapo kote ujenzi upo katika hatua za ukamilishaji.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.