Vitabu 47,930 vya kabidhiwa kwa halimashauri ya manispaa ya Ilemela ili kuboresha sekta ya elimu pamoja na kuondokana na changamoto ufundishaji na ujifunzaji.
Hayo yalibinishwa na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. John Mongella aliposema hauwezi kuzungumzia maendeleo bila ya elimu hasa ya msingi hivyo amekabidhi vitabu hivyo vya kusoma, kuandika, afya ya mazingira, michezo na sanaa, maarifa ya jamii na kingereza kwa ajili ya shule za msingi ili kuleta chachu ya usomaji kwa wanafunzi wa darasa la kwanza, pili na tatu.
Pia aliwataka wakuu wa shule kuhakikisha wanafunzi wanagawiwa vitabu na sio kuvifungia stoo ama kuviacha vikazagaa bali waazimishwe wanafunzi kwa utaratibu unaofaa na vitumike hata kwa vizazi vingine.
" Kila mtoto anatakiwa kuwa na kitabu kimoja wapewa hivyo vitabu hatutaki kukutana na watoto wasiojua kusoma hasa wa darasa la kwanza hadi la tatu na wakuu wa shule wenye tabia za zamani za kufungia vitabu stoo kila ukienda anatoa vilevile na kusema amenunua vipya waache wakibainika hatua kali zitachukuliwa dhidi yao "alisema Mongella .
Pia aliwataka kuacha tabia ya kuwarejesha nyumbani watoto kwa namna yoyote endapo akifanya hivyo aanze kuandika barua ya kuacha kazi kwanza ndipo achukue jukumu la kumrudisha mtoto nyumbani aidha kwa kukosa viatu, nguo ama sababu yoyote Kwani katika sera ya mtoto haki moja wapo ni kupata elimu.
Aliongeza kuwa lengo kuu ni kuondokana na watoto wasiojua kusoma, kuhesabu na kuandika hivyo kwa Mkoa wote wa Mwanza wamepokea vitabu 500,446, vyenye thamani ya sh. 1,251,115,000 hivyo ni jukumu lililopo ni kuvitumia .
Mongella alisema wakati umefika wa walimu, maofisa elimu kata na wadhibiti ubora wa shule kuzingatia ufatiliaji ubora wa utoaji elimu ufundishaji na usomaji wa watoto ili kuleta uelewa na matokeo mazuri.
" Hasa hawa maofisa elimu kata wamejijengea tabia ya kudhani wao wapo likizo mwaka mzima kazi yao ni kuzungukazunguka na kutoa macho tu na kutokuwa na maana ya ufanyaji kazi wao zaidi ya kuwa vyanzo vya watoto kufeli na upatikanaji wa ziro mashuleni" alisema Mongella.
Kwa upande wake, Ofisa elimu Mkoa Mwl. Michael Ligola alisema watahakikisha ndani ya wiki moja shule zote zitakuwa vimepata vitabu na kuwataka walimu wote waliokuwa wanalalamikia upungufu wa vitabu kuvitumia ipasavyo vitabu hivyo na kujituma katika utendaji kazi wao ili kuijenga vyema sekta ya elimu .
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.