Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza imefanya kikao kazi na viongozi na watendaji wa Halmashauri za Mkoa huo kwa lengo la kuwajengea uwezo kuhusu ujio wa Daftari la Makazi na Bima ya Afya kwa Wote.

Akifungua kikao hicho, Katibu Tawala wa Mkoa wa Mwanza Ndugu Balandya Elikana amesema Daftari la Makazi linalenga kuwasajili wananchi wote kwa ngazi ya kaya ili kurahisisha utambuzi na upatikanaji wa huduma za kijamii.

Amesema Wenyeviti wa Mitaa na Vijiji watakuwa wahusika wakuu wa kusimamia madaftari hayo, huku wananchi wakitakiwa kuhakikisha wanajisajili.

Aidha amesisitiza kuwa ni wakati sasa kwa viongozi na watendaji kwenda kutoa elimu kwa wananchi.

Ndugu Balandya ameongeza kuwa Bima ya Afya kwa Wote tayari imezinduliwa na Waziri wa Afya na kwamba juhudi zinaendelea kuhakikisha wananchi wanapata elimu kuhusu huduma 372 zinazopatikana kuanzia ngazi ya zahanati hadi mkoa kupitia kitita cha jamii.

Kwa upande wake, Meneja wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) Mkoa wa Mwanza Bw. Jarlath Mushashu amesema Mkoa ulizindua rasmi uhamasishaji wa elimu ya bima tarehe 17 Desemba, 2025 ili kila mwananchi apate uelewa wa mfuko huo.

Ameeleza kuwa Bima ya Afya kwa Wote itasogeza huduma karibu na wananchi na kuwezesha usajili wa bima kwa makundi mbalimbali ikiwemo kaya na mashirika huku mfumo wa huduma ukiwa ni wa kulipia kabla ya kupata huduma.

Amefafanua kuwa kaya yenye watu kuanzia mmoja hadi sita italipia Tshs. 150,000 kwa mwaka, ambapo wanufaika watasajiliwa kwenye mfumo maalumu unaosomana na mifumo mingine ya Serikali.

Kikao kazi hicho kilichowahusisha Mameya, Wenyeviti, Wakurugenzi wa Halmashauri pamoja na Maafisa Mipango, Utumishi na Waweka Hazina, pia kimejumuisha mafunzo ya Mpango wa Ufadhili Mbadala unaoratibiwa na Wizara ya Fedha.

Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.