HALMASHAURI ZISIZOFANYA VIZURI MPANGO WA LISHE ZIANDIKIWE BARUA KALI: RAS BALANDYA
*Asema ukosefu wa Lishe unachangia kushuka kwa ufaulu shuleni*
*Ahimiza Halmashauri zote kutii agizo la Mpango wa lishe*
*Kwimba kinara wa chakula shuleni*
Katibu Tawala wa Mkoa wa Mwanza Balandya Elikana ameagiza Halmashauri zilizolega lega kutekeleza mpango wa lishe shuleni zichukuliwe hatua ya kuandikiwa barua kali.
Akizungumza leo Machi 05, 2024, Balandya amesema mwanafunzi anaposhinda bila kula shuleni ufuatiliaji wa masomo unashuka na hatimaye kufanya vibaya katika masomo yake.
"Nawasihi sana viongozi wenzangu hili suala la lishe tukalisimamie vizuri, Serikali imeboresha miundombinu ya elimu ni lazima iende pamoja na ufaulu wa kiwango," amesisitiza Mtendaji huyo wa Mkoa wakati wa kikao kazi cha Kamati ya Lishe.
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Thomas Rutachunzibwa amebainisha kuwa bado kunahitajika mkazo wa kuelimishana licha ya ukweli hali za kimaisha zinachangia mtoto chini ya miaka 5 kukosa lishe bora.
"Wakina mama walio wengi ndiyo wazalishaji wa chakula cha familia, kuelemewa na shughuli za kusaka kipato anajikuta mtoto hamnyonyeshi inavyotakiwa na tutambue maziwa ya mama yana virutubisho vingi," Mganga Mkuu wa Mkoa.
Afisa Lishe wa Mkoa Sophia Lugome, amesema jumla ya watoto 85,683 wa miezi 6-59 wamepatiwa matone ya Vitamin A na watumishi 532 wamejengewa uwezo kuhusiana na elimu ya Lishe.
"Ulaji wa chakula shuleni ni 75.2% kwa Mkoa mzima hapo bado kuna changamoto kwani inaonesha Halmashauri nyingi bado zina suasua katika uhamasishaji wazazi kuchangia mlo kwa wanafunzi," Afisa Lishe.
Amesema ni wilaya ya Kwimba pekee ambayo inaendelea kufanya vizuri suala la wanafunzi kula shuleni.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.