Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango ameagiza ifikapo mwishoni mwa mwezi februari 2023 kuanza kutolewa kwa huduma za Afya kwenye Kituo cha Afya Igalla wilayani Ukerewe ili wananchi wa eneo hilo wapate huduma muhimu ya afya jirani na makazi yao.
Dkt. Mpango ametoa agizo hilo mapema leo Wilayani Ukerewe alipofika kukagua ujenzi wa Kituo hicho kilichofikia zaidi ya Asilimia 95 ya ujenzi huku kikigharimu zaidi ya Milioni 492 ambapo kinatarajiwa kuwanufaisha wananchi zaidi ya elfu 17,000 kutoka kwenye kata ya Igalla na kata za jirani za Bwiro, Mukituntu na Nduluma.
Akizungumza na wananchi, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Mpango amesema serikali itaendelea kufanya jitihada za kila namna kuajiri watumishi wa Afya kila wakati ili wakidhi mahitaji na amewataka wananchi kutunza amani ili wawe na uhuru wa kufanya kazi zitakazowainua kiuchumi.
Vilevile, ametoa rai kwa wananchi kuendelea kufanya kazi kwa bidii ikiwa ni pamoja na kutumia mvua vema katika kilimo ili wapate vyakula kwa ajili ya mahitaji yao na wawe na tabia ya kuweka akiba pamoja na kutunza Mazingira kwa kupanda miti kama sehemu ya Maisha yao.
Hata hivyo, amekemea tabia ya kuwapa mimba wanafunzi katika umri mdogo huku akibainisha kuwa matatizo kama ugonjwa wa Fistula yanatokana na uzazi katika umri mdogo na badala yake amewataka wazazi kuhakikisha watoto wao wanasoma kwa bidii.
Naibu Waziri wa TAMISEMl, Mhe. David Silinde amemshukuru Makamu wa Rais kwa kufika kwenye ujenzi huo ambao umetekelezwa vema kwa kutumia fedha za Mapato ya ndani kutokana na maelekezo ya viongozi wakuu wa nchi kupitia Wizara hiyo.
Kuhusu Vifaa Tiba, Mhe. Silinde amesema Vifaa Tiba vitaletwa kwenye kituo hicho cha Afya mara moja ili wananchi waweze kupata huduma za afya zilizo bora na kwa wakati tofauti na siku za nyuma ambapo walilazimika kusafiri umbali mrefu kufuata huduma hizo.
Naye, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya Ukerewe Emmanuel Sherembi amesema tayari Halmashauri hiyo imepokea watumishi 58 wapya na kwamba kwenye kituo hicho watapata watumishi akiwemo Mganga kwa kipaumbele ili huduma zianze mara moja.
Mganga Mkuu wa Wilaya ya Ukerewe, Dkt. Getela Nyangi amesema Ujenzi wa Kituo cha Afya Igalla utasaidia kupunguza gharama za usafiri kwa wananchi waliokua wakifuata siku huduma za Afya, Kupunguza msongamano katika Hospitali ya Wilaya pamoja na kupunguza idadi ya Vifo kutokana kupata huduma hiyo jirani.
Aidha, Dkt. Nyangi amewasilisha Ombi Maalumu kwa Mhe. Makamu wa Rais la kununuliwa vifaa tiba vya kisasa, Jenereta, Jengo la kufulia pamoja na wodi ya wanaume ili kukamilisha huduma zote kwenye kituo hicho kwani kwa upande wa majengo yanatarajiwa kukamilika ifikapo Disemba 20, 2022.
Awali, Dkt. Philip Mpango alikagua na kufungua Mradi wa Shule ya Sekondari ya Ukerewe iliyojengwa kwa Tshs Bilioni 1.1 kutoka Serikali kuu ambapo amewapongeza viongozi wa Wilaya hiyo kwa Utekelezaji wa mradi huo muhimu kwa maendeleo ya Sekta ya Elimu na akawataka kukamilisha Ujenzi wa Maabara ya fizikia.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.