Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda ameitaka Halmashauri ya Wilaya ya Magu kukamilisha miradi Saba (7) ya Ujenzi wa Madarasa na matundu ya Vyoo katika shule za msingi ndani ya Siku 14.

Ametoa wito huo mapema leo wilayani humo katika nyakati tofauti wakati akikagua utekelezaji wa miradi ya ujenzi wa vyumba vya Madarasa na Matundu ya Vyoo kwa gharama ya Tshs. Bilioni 1.4 fedha kutoka serikali kuu.

Mkurugenzi wa Halmashauri asilale usingizi, akilala miradi haitakamilika na hili pia Menejimenti ya Halmashauri pia hili linawahusu msilale pia. Amesema Mkuu wa Mkoa.

Aidha, ametoa rai kwa wazazi na walezi kuhakikisha wanawapelekea watoto shuleni pasipo kuchelewa ili malengo ya serikali ya kuwapatia elimu watoto itimie kwani hadi sasa wilaya hiyo wameripoti wanafunzi kwa 50% tangu shule zifunguliwe.

“Wazazi ambao hamjawapeleka watoto shuleni nimekuja kuwakumbusha muwapeleke wakaandikishe na Mkoa huu tumefikisha 72% za uandikishaji na tunataka kufikia 100% hivyo asituangushe yeyote na mwenye changamoto amuone kiongozi wa kitongoji au kijiji kwa msaada.” Mhe. Mtanda.

Vilevile, ametumia wasaa huo kumshukuru Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Hassan kwa kuajiri watumishi elfu 1200 mkoani humo katika sekta za Elimu na Afya huku kwa Magu wakipokea 142.

Akitoa taarifa ya ujenzi wa shule ya Msingi Muungano katika Kata ya Kisesa Mwalimu Ruth Simon amesema ujenzi wa Vyumba 7 vya madarasa na matundu 12 ya vyoo utakamilika ifikapo februari 15, 2026 kwani changamoto zilizowakabili wameshazitatua ikiwemo ugumu wa kumpata fundi.

“Ninawataka wananchi wa Magu mdumishe amani na upendo, hakuna maendeleo mahali popote bila kuwa na amani hata katika familia haiwekezani hivyo basi tuhakikishe tunadumisha maelewano na umoja.” Amesisitiza Mkuu wa Mkoa.

Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.