Katibu Tawala Mkoa wa Mwanza Bw. Balandya amezipongeza na kutoa wito kwa Mamlaka za usimamizi wa huduma za Maji nchini kuendelea kuzijengea uwezo taasisi za Maji hususani katika kugawa rasilimali, kukabiliana na dharura, na kuhakikisha uendelevu wa kifedha na kiutendaji.
Bwana Balandya amesema hayo leo tarehe 02 Septemba, 2025 wakati akifungua warsha ya mafunzo kuhusu usimamizi wa mashirika ya maji yaliyoandaliwa kwa ushirikiano kati ya Wizara ya Maji, taasisi ya IHE Delft kutoka Uholanzi, Hamburg Wasser kutoka Ujerumani na GIZ pamoja na mashirika ya maji nchini Tanzania.
Aidha, amezipongeza mamlaka hizo kwa kuwa nyenzo ya mafunzo ya vitendo katika kusimamia huduma za maji kwa ufanisi mathalani katika eneo la uandaaji wa mipango mikakati ya muda mrefu na mfupi katika kuhakikisha huduma za maji kwa jamii zinakua bora siku hadi siku.
“Usimamizi wa huduma za maji ni zana madhubuti ya kujifunza jinsi ya kusawazisha mahitaji ya sasa na mipango ya muda mrefu katika utoaji wa huduma za maji kwa wananchi,” amesema RAS Balandya.
Kadhalika, amewasisitiza washiriki wa mafunzo hayo kuhudhuria kikamilifu na kujibidiisha katika kupata ujuzi mpya utakaofundishwa hususani masuala ya teknolojia za kisasa kwenye maji ili watakaporudi katika mamlaka zao wakasaidie kuboresha maisha ya wananchi.
“Mnapoanza safari ya warsha nawahimiza mshiriki kikamiliífu, muwe wazi, mshirikiane na mjitahidi zaidi kutoa changamoto kwa uhuru na mtumie nafasi hii kikamilifu ili mkaboreshe maisha ya mamilioni ya watanzania wanaotegemea huduma bora za maji kutoka kwetu.” Amesema Ndg. Balandya.
Naye, Mkurugenzi wa ufatiliaji na uwekezaji kutoka Wizara ya maji Bi. Diana Kimario amesema matokeo ya mafunzo hayo yanaweza kusaidia kuandaa kukabiliana na changamoto pamoja na uwajibikaji kwa wananchi wanaotumia huduma za maji.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.