MATOKEO YA SENSA YA WATU NA MAKAZI NI MUHIMU KWA KUPANGA MIRADI NA HUDUMA KWA JAMII-RC MAKALLA.
*Ampongeza Rais Samia kwa kufanikisha Sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022*
*Asisisitiza makundi ya vijana yaelimishwe ili watambue fursa za kiuchumi zilizopo maeneo yao*
*Ashauri mipango imara ifanyike ya huduma zote za msingi kwa wananchi na kuondoa umasikini wa kipato*
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. CPA Makalla amesisitiza kuwepo na kipaumbele wa utoaji elimu ya matokeo ya Sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022 kwa makundi ya vijana ambao ndiyo nguvu kazi ya Taifa ili watambue fursa za kiuchumi zilizopo maeneo yao.
Akifungua leo Oktoba 13, 2023 Mafunzo ya matokeo ya Sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022 kwenye ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mhe Makalla amesema makundi ya vijana wakipata elimu ya kutosha itawasaidia kujikomboa kiuchumi kwa kutumia vizuri fursa zinazowazunguka.
"Kuna kasumba ya kundi la vijana kupenda kukimbilia maeneo ya mjini kutafuta kazi mbalimbali na kujikuta wakiwacha fursa za kiuchumi zilizopo maeneo yao, hivyo kwa kupitia elimu watakayopata itawafumbua macho na kujipatia kipato," CPA Makalla.
Aidha, amebainisha kuwa kwa Mkoa wa Mwanza takwimu zinaonesha kuna idadi ya watu milioni 3.7 huku Halmashauri ya Nyamagana ikiongoza kwa idadi kubwa ya watu, hivyo ni wajibu kwa wahusika kuja na mipango kuanzia ngazi ya chini.
"Hivi sasa nimeanza kusikiliza kero za wananchi, nashuhudia kundi kubwa la vijana wakilalamikia kukosa kazi na kuomba nafasi mbalimbali kwenye majeshi yetu,hii inadhihirisha bado kuna jambo la msingi la kuwasaidia", amesisitiza Mhe.Makalla wakati akizungumza na washiriki wa mafunzo hayo.
Vilevile, amemshukuru Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu kwa kufanikisha Sensa ya watu na makazi kwa kutoa vishkwambi vilivyotumika nchi nzima vilivyossidia kazi ya Sensa kufanyika kwa ubora na umakini.
Awali akizungumzia malengo ya mafunzo hayo Afisa kutoka Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali, Benedict Mugambi amebainisha malenngo ya Sensa ni Serikali kupata hesabu halisi ya wananchi wake ili iweze kuweka mipango imara ya kuwahudumia kulingana na maeneo wanayoishi,hivyo wananchi pia wana wajibu wa kutumia vizuri matokeo hayo ili kuweza kujiinua kiuchumi.
"Tumetoa mafunzo haya kwa Wilaya za Nyamagana na Ilemela na leo tunatoa ngazi ya Mkoa,lengo ni kuja na matokeo chanya kwa kuona namna ya kutoa huduma bora kwa wananchi na pia fursa za kiuchumi zilizopo maeneo husika,"Benedict Mugambi, Meneja Idara ya shughuli za kitakwinu.
Kwa mujibu wa matokeo ya Sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022, Tanzania Ina jumla ya watu milioni 61.7 huku Mkoa wa Njombe ukiwa na idadi ndogo ya watu 900,000 na kwa upande wa Zanzibar Mkoa wa kusini Unguja ukiwa na idadi ndogo ya watu 200,000.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.