MIRADI YA UBORESHAJI WA MIUNDOMBINU YA MAJISAFI NA MAZINGIRA YAKABIDHIWA
Katibu Tawala wa Wilaya Misungwi Bw. Josaphati Mshaghati amewataka Wananchi kutunza na kulinda miundombinu ya afya inayotekelezwa na Serikali kwa kushirikiana na washirika mbalimbali ili iweze kudumu kwa muda mrefu na iwahudumie wakazi wa maeneo hayo Kwa muda mrefu.
Katibu Tawala huyo ameyasema hayo Novemba 28, 2024 wakati akizindua mradi wa Xylem Watermark chini ya Shirika losilo la Kiserikali la Americares katika Zahanati ya Sanjo iliyopo Kata ya Usagara Wilayani Misungwi, alipokuwa akimuwakilisha Katibu Tawala Mkoa wa Mwanza.
Ameongeza kuwa katika jitihada zinazofanywa na Serikali ya awamu ya sita ni kuhakikisha kuwa wananchi wanaboreshewa miundombinu Afya na kufungua milango kwa wafadhili mbalimbali.
"Tunawashukuru wafadhili wetu Kwa kazi kubwa lakini pia muangalie na maeneo mengine yenye changamoto mbalimbali za kiafya kwani uwepo wenu katika Mkoa wetu huu una tija kubwa kwa maendeleo ya Serikali na wananchi wake".
Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Dkt. Jesca Lebba ameushukuru Uongozi wa Shirika la Americares kwa kuendelea kuisaidia sekta ya Afya hususani kwa vituo mbalimbali vya Afya.
Watumishi wa Afya tuzingatie ubora wa huduma, kama Mkoa tunaendelea kufanya jitihada ili tulete maombi ya vituo vingine, kinachotakiwa sasa hivi ni ubora wa huduma, uwepo wa miundombinu kama ya Majisafi na salama katika vituo vya Afya kutasaidia kuboresha huduma kwa wananchi. Ameongeza Dkt. Leba
Shirika lisilo la Kiserikali la Americares limefadhili vituo mbalimbali ikiwa ni pamoja na Zahanati ya Lumala iliyopo Wilaya ya Ilemela, Zahanati ya Sahwa iliyopo Wilaya ya Nyamagana, Zahanati ya Sanjo iliyopo Wilaya ya Misungwi, Zahanati ya Kiliwi ipo katika Wilaya ya Kwimba, kituo Cha Afya Cha Sima kilichopo Wilaya ya Sengerema na kituo cha Afya cha Nyakalilo kilichopo Halmashauri ya Wilaya ya Buchosa.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.