Mradi wa kurejesha Ardhi iliyoharibika wasaidia kuondoa uhaba wa chakula Magu
Wananchi Wilayani Magu wamelishukuru Shirika la Kimataifa la Maendeleo ya Kilimo (IFAD) kwa kuwaletea miradi inayosaidia kurejesha Ardhi iliyoharibika ambapo wamesema imewahakikishia upatikanaji wa chakula cha kutosha na usalama wa chakula kwenye kaya zao.
Hayo yamebainika leo kwenye kijiji cha Lumeji kata ya Sukuma-Magu wakati wa ziara ya Makamu Rais wa shirika hilo alipotembelea mradi wa ufugaji Kondoo ambapo wananchi wamebainisha kuwa mradi huo umewasaidia pamoja na kuuza Kondoo kutokana na kuzaliana vilevile unawapatia mbolea ya asili wanayoitumia kwenye kilimo na kuongeza uzalishaji.
Akizungumza kwa niaba ya kikundi cha ufugaji Kondoo Ndugu Ernest Pamba amesema awali kwenye eneo lao walikua wanakumbwa na changamoto ya mabadiliko ya tabia nchi lakini kupitia mradi huo wameweza kuuza kondoo na kupata mbolea ya asili wanayoitumia kwenye mashamba.
Vilevile, ametoa wito kwa Serikali kendelea kuleta miradi yenye tija kama hiyo na kuboresha kwa kuipanua kwenye maeneo mengi ili wananchi walio wengi wapate kujifunza teknolojia na kuboresha hali ya usalama wa chakula na kuhakikisha upatikanaji wa chakula cha kutosha.
Makamu Rais wa Shirika hilo Donal Brown
amesema amefurahishwa na utekelezaji mzuri wa miradi wilayani humo na ameahidi katika wakati mwingine wataangalia namna ya kuboresha kama vile kuwaletea miradi ya mabwawa ya maji ili kukabiliana na ukame.
"Nawapongeza kwa mradi mzuri wa ufugaji kondoo mmeufanya vizuri nami hii ndio taaluma yangu, nimegundua kuwa tatizo kubwa hapa ni maji katika uboreshaji wa miradi yetu baadae tutaangalia namna ya kuleta mabwawa."
Bwana Brown.
Naibu Katibu Mkuu kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais Dkt. Sweetbert Mkama ametoa wito kwa wananchi kutunza miradi hiyo huku akibainisha kuwa itawasaidia kwenye nyanja mbalimbali za chakula na uhifadhi wa mazingira na vilevile ametumia wasaa huo kuwaomba IFAD kuleta miradi mingine kwa ajili ya kusaidia jamii hiyo kwani mahitaji ni makubwa bado.
Emil Kasagara aliyemwakilisha Katibu Tawala wa Mkoa wa Mwanza ameishukuru Serikali ya awamu ya Sita kwa kuweka mazingira wezeshi ya wahisani kuja kusaidia wananchi na amefafanua kuwa mbolea inayopatikana kwenye mradi wa ufugaji kondoo inasaidia kuzalisha mazao na kuimarisha usalama wa chakula.
"Nchi kumi na mbili barani Afrika zinafadhiliwa na miradi mbalimbali ya uhifadhi wa mazingira, lakini mradi huu unaogharimu zaidi ya Bilioni 1 wilayani Magu umejikita kwenye sekta za ufugaji, kilimo na umwagiliaji na una lengo la kuimarisha upatikanaji wa chakula, kutunza mazingira na kuondoa utapiamlo. Amesema Joseph Kihaule mratibu wa miradi ya GEF IFAD- LDFS nchini.
Naye, Tabu Daudi mwanakikundi katika Shamba darasa la Mihogo Nyang'hanga amebainisha kuwa mradi huo umesaidia kuwapatia chakula cha kutosha kwani mbegu hiyo (TZ 130) inakomaa ndani ya miezi tisa tu tofauti na mbegu za asili walizokua wanalima siku za nyuma.
"Tulikua na mbegu ambazo zilikua ngumu kukomaa ila sasa kwa mbegu hii ya kisasa imetupa chakula cha kutosha na hata kuweza kuuza kingine na kupata fedha za kujikimu, kwakweli hii mbegu imefukuza njaa na tunawashukuru sana maafisa Ugani kwa kutuongoza vizuri", amesisitiza.
Masalu Issa amesema amefanikiwa kulima shamba la Viazi kutokana na uwepo mradi wa umwagiliaji na kwamba yupo kwenye mpango wa kulima Viazi lishe kwani shirika hilo limeleta maji ya kutosha kuhudumia mashamba yao naye ana malengo ya uzalishaji mkubwa zaidi kwenye siku za usoni.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.