MWANZA, SIMIYU ZANG'ARA UTAMILIFU DARASA LA SABA KANDA YA ZIWA
Katibu Tawala Mkoa wa Mwanza Ndg. Balandya Elikana leo Mei 30,2025 ametangaza matokeo ya mtihani wa Utamilifu wa darasa la saba Kanda ya ziwa huku mkoa wa Simiyu ukishika nafasi ya kwanza, Mwanza ikiwa ya pili na Shinyanga ikishika nafasi ya tatu.
Akizungumza na Maafisa elimu kutoka mikoa 6 ya Kanda ya ziwa kwenye ukumbi wa Ofisi ya mkuu wa mkoa, Balandya ametoa Rai bado juhudi ya ziada inabidi kufanyika kutokomeza utoro na kupandisha viwango vya ufaulu kwa masomo ya Hisabari na Kiingereza.
"Kwa mujibu wa matokeo ya mtihani huu inaonesha asilimia 70.1 ya wanafunzi wamefeli somo la Hisabari na asilimia 73.61 hawajafanya vizuri somo la Kiingereza, sasa ni wajibu wetu walimu kukabiliana na changamoto hii kabla ya Septemba mwaka huu", Balandya.
Aidha, amewataka walimu kukaa chini na kutokomeza hali ya utoro shuleni ambayo inaonesha kuwa sugu mwaka hadi mwaka.
Katibu Tawala Balandya pia amewataka walimu ambao shule zao hazijafanya vizuri katika mtihani huu wa Utamilifu kwenda kuongeza bidii ili viwango vya ufaulu viongezeke.
Katika mkutano huo wa kutangaza matokeo, Katibu Tawala ametumia wasaa huo kuzipongeza Halmashauri za Kwimba, Misungwi, Nyamagana, Ilemela na Bariadi kwa kufanya vizuri wanafunzi kwenye mitihani hiyo.
Katika mtihani huo wa Utamilifu, Mkoa wa Kagera umeshika nafasi ya nne, Geita ni ya Tano na Mara wameshika nafasi ya sita.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.