PPRA YAWANOA WARATIBU WA WASH MFUMO WA NeST
Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma-PPRA inaendesha mafunzo juu ya Mfumo wa Usimamizi wa Ununuzi wa Umma (NeST) kwa Maafisa ununuzi, Waratibi na Wasimamizi wa mradi wa Programu za Uendelevu wa Usambazaji wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (WASH) ngazi ya Mkoa na Halmashauri Mkoani Mwanza.
Mafunzo hayo yaliyoanza rasmi leo Februari 06, 2025 katika ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza yamefunguliwa na Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Mwanza Ndugu Kusirie Swai na amewataka washiriki hao kufanya manunuzi yote kupitia Mfumo wa NeST.
Ndg. Swai amesema Mkoa wa Mwanza ni miongoni mwa Mikoa inayotekeleza programu ya WASH ambapo utekelezaji wa Programu hiyo unahusisha kufanya manunuzi mbambali kupitia Mfumo wa NeST hivyo ni muhimu kwa wahusika wa manunuzi kuwa na uelewa wa kutosha kuhusu matumizi ya mfumo huo.
“Ndugu Washiriki wa mafunzo, kutokana na umuhimu wa utekelezaji wa programu, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa imeandaa mafunzo haya ili kuwajengea uwezo wafawidhi wa vituo vitakavyotekeleza mradi kwa mwaka 2024/2025”. Ndugu Swai.
Aidha, amesema mafunzo hayo ni muhimu kwao na wanapaswa kuyatilia maanani ili iwasaidie katika kuwezesha utekelezaji wa programu kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu katika ununuzi wa umma.
Kwa upande wake Mganga Mkuu Mkoa wa Mwanza Dkt. Jesca Lebba amewapongeza wadau hao kwa kazi nzuri wanayofanya katika kusambaza maji na huduma ya usafi wa mazingira Mkoani humo na akatoa wito kwao kuhakikisha wanakuwa makini ili wakayatumie mafunzo hayo katika kufanya manunuzi kwa njia ya kielektroniki bila kukwama.
Aidha, Mganga Mkuu wamesisitiza umuhimu wa kufuata miongozo ya utekelezaji wa kazi hizo ili kuhakikisha miradi kama vyoo, vichomea taka, matenki ya maji na vinginevyo viweze kukamilika kwa wakati na kwa ubora unaokusudiwa.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.